Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, ameieleza Bunge kuwa hali ya usalama katika mipaka ya nchi imeendelea kuwa shwari na yenye utulivu katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26, huku vyombo vya ulinzi vikiendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ulinzi wa taifa unaimarika zaidi.

Akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri huyo amesema Tanzania ina jumla ya kilomita 5,923.41 za mipaka, inayojumuisha mipaka ya nchi kavu, anga pamoja na eneo la maji.

Kwa mujibu wa Waziri Nyansaho, mipaka ya nchi kavu ya Tanzania inagusa mataifa ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Uganda na Zambia, huku upande wa bahari ya Hindi Tanzania ikipakana na visiwa vya Comoro na Shelisheli.

Ameeleza kuwa katika kipindi hicho hakujakuwa na matukio yoyote makubwa yaliyoashiria uvunjifu wa amani kati ya Tanzania na nchi jirani, jambo linaloonesha uimara wa diplomasia na ulinzi wa mipaka ya taifa.

Hata hivyo, Waziri Nyansaho amesema bado kuna changamoto kadhaa za kiulinzi na kiusalama katika baadhi ya maeneo ya mipaka, ikiwemo uharibifu wa alama za mipaka, ukosefu wa miundombinu ya barabara za ulinzi katika baadhi ya maeneo, pamoja na uharibifu wa baadhi ya miundombinu hiyo iliyopo.

Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya changamoto zinatokana na hali ya ndani ya nchi jirani zinazopakana na Tanzania, jambo linalohitaji ufuatiliaji wa karibu na ushirikiano wa kikanda katika kuhakikisha usalama unaendelea kudumishwa.

Waziri huyo ameihakikishia Bunge kuwa Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama itaendelea kuimarisha ulinzi katika mipaka yote ya nchi kwa lengo la kulinda raia, mali zao na maslahi ya taifa kwa ujumla.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...