Miamala ya uwekezaji wa kidijitali kupitia ushirikiano kati ya Mixx by Yas na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeongezeka kutoka Shilingi milioni 840 hadi Shilingi bilioni 6.9 ndani ya mwaka mmoja, huku maelfu ya vijana wa Kitanzania wakijiunga na masoko ya mitaji kupitia simu za mkononi.
Ukuaji huo umebainishwa wakati wa hafla ya ushirikiano kati ya Mixx na DSE iliyofanyika Dar es Salaam chini ya kaulimbiu ya “Nafasi ya Malipo ya Kidijitali katika Kuendesha Kizazi Kijacho cha Wawekezaji.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Bi. Angelica Pesha, alisema kampuni hiyo inaendelea kupanua huduma zake zaidi nje ya miamala ya kifedha kwa njia ya simu kwa kuwezesha Watanzania kujenga utajiri kupitia suluhisho rahisi za uwekezaji kidijitali.
“Siku zote tumekuwa tukiamini kuwa ujumuishaji wa kifedha haujakamilika bila ujumuishi kwenye uwekezaji,” alisema Pesha. “Haitoshi watu kutuma na kupokea fedha pekee; tunapaswa kuwawezesha kukuza utajiri wao, kumiliki mali na kushiriki kikamilifu katika masoko yetu ya mitaji.”
Alisema kuunganishwa kwa mfumo wa Hisa Kiganjani wa DSE ndani ya Mixx Super App kumerahisisha upatikanaji wa fursa za uwekezaji kwa kuwawezesha watumiaji kuwekeza moja kwa moja kupitia simu zao bila usumbufu.
Hisa Kiganjani ni jukwaa la kidijitali la DSE linalowezesha Watanzania kununua hisa na kushiriki katika masoko ya mitaji kupitia vifaa vya simu.
Kwa mujibu wa Pesha, idadi ya wawekezaji wanaotumia jukwaa hilo imeongezeka kutoka 6,800 hadi 32,000 ndani ya mwaka mmoja, huku miamala ikiongezeka kutoka 8,600 hadi 41,500.
“Ukuaji huu unaonesha kuwa pale ambapo huduma zinarahisihwa, ushiriki wa watu huongezeka kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Pesha aliongeza kuwa huduma kama Kibubu, Bustisha pamoja na suluhisho mbalimbali za uwekezaji kidijitali, zinaonesha dhamira pana ya Mixx ya kuwa taasisi kamili ya kifedha inayolenga kuwawezesha Watanzania kiuchumi.
Alisema kuongezeka kwa ushiriki wa wawekezaji wa kizazi cha Gen Z ni uthibitisho kuwa uwekezaji si jambo la watu wachache tena.
“Huhitaji tena kuwa na fedha nyingi ili kuanza kuwekeza. Kupitia majukwaa ya kidijitali, fursa za uwekezaji sasa zinapatikana kwa kila mtu,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela, alisema Tanzania inashuhudia mabadiliko makubwa katika namna wananchi wanavyoshiriki kwenye masoko ya kifedha kutokana na ubunifu wa kidijitali.
“Je, vipi kama mustakabali wa uwekezaji nchini Tanzania hautajengwa kwenye korido za masoko ya hisa bali kwenye simu za mkononi?” alihoji Nalitolela. “Nchi nzima, watu ambao hapo awali walikuwa nje ya masoko ya mitaji sasa wanashiriki kutokana na upatikanaji kuwa wa kidijitali zaidi.”
Alisema ushirikiano kati ya DSE na Mixx umeondoa vikwazo kwa kuwawezesha wawekezaji kuweka fedha kwenye akaunti zao papo hapo kupitia huduma za fedha kwa simu, hatua inayorahisisha na kuharakisha miamala ya uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Alfred Mkombo, aliwataka Watanzania kutumia fursa zilizopo kwenye masoko ya mitaji kupitia uwekezaji katika hisa na hatifungani ili kupata mitaji na kukuza biashara zao.
Mkombo alisema kuwa kuongezeka kwa ushiriki wa vijana wa Kitanzania kwenye majukwaa ya uwekezaji ni matokeo ya mafanikio ya jitihada zinazoendelea za kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na masoko ya mitaji kwa wananchi kote nchini.
Ushirikiano kati ya Mixx na DSE unatarajiwa kuongeza kasi ya ushiriki wa wawekezaji wa kawaida huku Tanzania ikiendelea kusukuma ajenda ya uchumi jumuishi wa kidijitali na uwezeshaji mpana wa kifedha.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...