Na Belinda Joseph-Dodoma.

Masuala ya usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na makundi maalum pamoja na mapambano dhidi ya mfumo dume yameendelea kupewa uzito nchini, huku wadau mbalimbali wakisisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kwa pamoja kujenga mazingira yenye haki na usawa kwa wote.

Hayo yamejadiliwa Mei 14, 2026 Jijini Dodoma katika mjadala ulioandaliwa na Aga Khan Foundation kupitia mradi wa Tuinuke Pamoja, uliowakutanisha viongozi wa dini, maafisa maendeleo ya jamii, wazee wa mila pamoja na vikundi vya wanawake vinavyowezeshwa na mradi huo kwa Wilaya za Bahi, Dodoma Jiji na Chamwino.

Akizungumza katika mjadala huo, Zaibu Mmari ambaye ni mratibu wa masuala ya kijinsia wa Aga Khan Foundation Makao Makuu Dar es Salaam, amesema lengo la mradi huo ni kuchochea usawa wa kijinsia katika jamii, kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha mshikamano na kuleta mahusiano bora kupitia elimu na ushirikiano wa kijamii.

Amesema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa wanawake na wasichana barani Afrika wameachwa nyuma kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, jambo lililosababisha mradi huo kuelekeza nguvu kubwa kwa wanawake na wasichana kwa zaidi ya asilimia 70.

“Tunataka kuhakikisha kwamba usawa unaendana na haki, Fursa lazima zigawanywe kwa kuzingatia mahitaji ya kila kundi katika jamii, Pia tunawahimiza viongozi wa dini kutumia madhabahu na mimbari kufundisha kuhusu usawa wa kijinsia, kupinga mfumo dume na kukemea fikra mgando.”

Ameeleza kuwa mradi wa tuninuke pamoja unaratibiwa na Aga Khan Foundation ambayo ipo chini ya Aga Khan Development Network ambao ni mtandao wa maendeleo unaojihusisha na shughuli za kiuchumi, kijamii na kitamaduni chini ya jumuiya ya Waislamu wa Ismailia. Kupitia Aga Khan Foundation, taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi moja kwa moja na jamii katika kutambua changamoto na kushirikiana kutafuta suluhisho la pamoja.

Mradi wa Tuinuke Pamoja unafadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2027 katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma.

Afisa Mradi wa Tuinuke Pamoja katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Erick Maurid, alisema mradi huo unafanya kazi kwa karibu na vikundi vya wanawake, vijana pamoja na makundi maalum katika jamii ili kuvijengea uwezo wa kiuchumi na kijamii.

Amesema katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji, mradi ulifika Wilaya za Kondoa DC, Kondoa TC na Chemba, huku mwaka wa pili ukihusisha Wilaya za Bahi, Dodoma Jiji na Chamwino na mwaka wa tatu unatarajiwa kufikia Wilaya za Kongwa na Mpwapwa.

Ameeleza kuwa vikundi hivyo hutakiwa kusajiliwa kupitia maafisa maendeleo ya jamii katika halmashauri husika, huku mradi ukiwasaidia katika maeneo ya elimu ya biashara, ujasiriamali na usawa wa kijinsia.

“Mjadala huu unalenga kujenga mazingira bora katika jamii kwa kujadili masuala ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, elimu, utawala bora, HIV pamoja na haki za watu wenye ulemavu”.

Aidha amesema wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kufikia maendeleo, hivyo kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Katika mjadala huo, wazee wa mila kutoka Halmashauri za Bahi, Chamwino na Dodoma Jiji wamesisitiza umuhimu wa kulea watoto katika misingi ya usawa bila upendeleo wa kijinsia.

Wamesema viongozi wa serikali za mitaa wanapaswa kuwapa nafasi ya kutoa mawaidha katika mikutano ya vijiji ili kusaidia kurejesha maadili katika jamii, huku wakitoa rai kwa wazazi kuhakikisha watoto wa kike hawarubuniwi na kuingia katika mimba za utotoni.

Kwa upande wake, Ester Athanas kutoka Wilaya ya Bahi, amesema changamoto kubwa inayojitokeza vijijini ni mgawanyo usio sawa wa mali na urithi kati ya watoto wa kike na wa kiume.

Aidha ameeleza jinsi wanawake wengi ambavyo bado wananyimwa nafasi za maamuzi na kudharauliwa katika jamii kutokana na imani potofu na mifumo kandamizi.

“Ni muhimu kuondoa ukuta wa usiri kati ya mzazi na mtoto ili watoto waweze kueleza changamoto wanazokutana nazo kwa uhuru. Pia sheria ziangaliwe upya ili watoto wa ndani na nje ya ndoa waweze kupata haki sawa ya urithi.”

Naye Valentino Kibaja Mchungaji kutoka Wilaya ya Chamwino amewataka viongozi wa dini kuendelea kuhimiza ibada, maadili na elimu kwa usawa kwa watoto wa kike na wa kiume.

Amesema pia kuna umuhimu wa kuongeza ushirikishwaji wa viongozi wa dini katika mijadala ya kijamii ili kusaidia kujenga jamii yenye usawa, amani na mshikamano.

Mjadala huo umeonekana kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili namna bora ya kuondoa changamoto za kijinsia na kuhakikisha makundi yote katika jamii yanapata haki, fursa na ushiriki sawa katika maendeleo.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...