Na Aron Msigwa – Nairobi, Kenya

Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Fadhili Omary Nondo, ameungana na Maafisa Wakuu wa Majeshi na viongozi mbalimbali kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) akimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda katika ufunguzi rasmi wa zoezi la 14 la pamoja la Vituo vya Uamrishaji vya Kijeshi vya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki lijulikanalo kama Ushirikiano Imara 2026, uliofanyika leo Mei 14, 2026 jijini Nairobi, Kenya.

Zoezi hilo kubwa la kijeshi limekusanya washiriki kutoka nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini na Somalia kwa lengo la kuimarisha utayari, ushirikiano na uwezo wa vikosi vya ulinzi vya Jeshi, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, Wizara na taasisi za kiraia katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazolikabili eneo la Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo, Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (VCDF), Luteni Jenerali John Mugaravai Omenda, amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa EAC kuendelea kuimarisha mshikamano, ushirikiano na maandalizi ya pamoja katika kukabiliana na vitisho vinavyojitokeza, majanga mbalimbali pamoja na changamoto za kiusalama zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu wa kikanda.

Zoezi la Ushirikiano Imara 2026 limejengwa katika mazingira ya kinadharia ya nchi ya kufikirika ya “Jamhuri ya Pwani,” inayokabiliwa na mgogoro wa kisiasa huku likiangazia Operesheni za kusaidia Amani (PSO), Kupambana na Ugaidi (CT), Kupambana na Uharamia Baharini (CP) pamoja na Usimamizi wa Maafa (DM).

Katika mazoezi hayo, vikosi kutoka Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda, Uganda, Somalia na Sudani Kusini vitaonesha umahiri kupitia mafunzo mbalimbali katika eneo la Mawasiliano ya kimkakati, kubadilishana taarifa za usalama, uratibu wa operesheni, doria katika maeneo ya mijini pamoja na mbinu za utendaji katika mazingira hatarishi.

Mazoezi hayo yanalenga kuonesha kiwango cha juu cha taaluma, nidhamu na uwezo wa kiutendaji wa vikosi shiriki, sambamba na kuimarisha uwezo wa pamoja katika kulinda amani na usalama wa kikanda mipango ya pamoja ya kuzuia migogoro, kuimarisha utayari wa kukabiliana na majanga na kuboresha mifumo ya utoaji wa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.

Zoezi la Ushirikiano Imara 2026 linafanyika kwa kuzingatia Itifaki ya Ushirikiano wa masuala ya Ulinzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama kupitia upangaji na utekelezaji wa operesheni za pamoja zinazohusisha vyombo vya ulinzi na wadau wa kiraia.

Hafla hiyo ya ufunguzi imehudhuriwa pia na Msimamizi Mkuu wa zoezi hilo (Chief Umpire) ambaye pia ni Kiongozi wa kikosi cha Tanzania, Brigedia Jenerali Maneno Almasi Mabakila, Maofisa Waandamizi kutoka Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza, Wizara na Taasisi za Kiraia wanaoshiriki zoezi hilo.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...