Msimamizi
Mkuu wa Zoezi la 14 la Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Uamrishaji vya
Jumuiya ya Afrika Mashariki “Ushirikiano Imara 2026” Balozi Lindsay
Kiptiness akiwakaribisha viongozi na maafisa wa kijeshi kutoka nchi za
Kenya, Tanzania, Burundi, Uganda, Rwanda, Somalia na Sudani Kusini
wanaoshiriki zoezi hilo Jijini Nairobi leo Mei 11, 2026. Zoezi hilo
linalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda pamoja na kuongeza uwezo wa
pamoja wa kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazoikabili kanda
hiyo.
Na Aron Msigwa – Nairobi, Kenya
Msimamizi Mkuu wa Zoezi la 14 la
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Uamrishaji vya Jumuiya ya Afrika
Mashariki “Ushirikiano Imara 2026” Balozi Lindsay Kiptiness amesisitiza
umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea
kuimarisha umoja, ushirikiano na utayari wa pamoja katika kukabiliana
na majanga, vitisho na changamoto mbalimbali za kiusalama zinazoweza
kuhatarisha amani na utulivu wa kikanda.
Balozi Kiptiness amesema
hayo leo Mei 11, 2026 wakati wa mapokezi ya washiriki wa Zoezi la 14 la
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Uamrishaji vya Jumuiya ya Afrika
Mashariki “Ushirikiano Imara 2026” lililoanza rasmi Jijini Nairobi,
Kenya.
Zoezi hilo limewakutanisha viongozi na maafisa wa kijeshi
kutoka nchi za Kenya, Tanzania, Burundi, Uganda, Rwanda, Somalia na
Sudani Kusini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda pamoja na
kuongeza uwezo wa pamoja wa kukabiliana na changamoto za kiusalama
zinazoikabili kanda hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi amesema kuwa kufanyika kwa zoezi
hilo kuna umuhimu mkubwa katika kuimarisha mfumo wa usalama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, akibainisha kuwa mabadiliko ya hali ya usalama
duniani yanahitaji nchi wanachama kushirikiana kwa karibu zaidi katika
kulinda amani, utulivu na ustawi wa wananchi wake.
Aidha, amesema
migogoro na hali ya kutokuwa na utulivu katika maeneo mbalimbali
duniani, hususani Mashariki ya Kati pamoja na maeneo mengine yenye
migogoro, inaendelea kuathiri kwa namna mbalimbali uchumi, usalama na
maisha ya wananchi wa nchi za EAC. Amesema hali hiyo inaonesha umuhimu
wa kuendelea kuimarisha mshikamano wa kikanda, kubadilishana taarifa za
kiusalama na kuwa na mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto
hizo.
Balozi
Kiptiness ameongeza kuwa Zoezi la “Ushirikiano Imara 2026” ni jukwaa
muhimu linalowezesha taasisi za ulinzi na usalama za nchi wanachama
kuongeza uwezo wa uratibu wa operesheni, kuimarisha mipango ya kimkakati
na kujenga uaminifu miongoni mwa mataifa shiriki. Amesema hatua hiyo
inaakisi dhamira ya pamoja ya nchi za EAC katika kuhakikisha ukanda huo
unaendelea kuwa wa amani, usalama na utulivu.
Aidha,
amesisitiza kuwa amani na usalama ni msingi muhimu wa maendeleo
endelevu, ushirikiano wa kikanda, biashara na ustawi wa kiuchumi ndani
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki akitoa wito kwa nchi wanachama kuendelea
kuwekeza katika mipango ya pamoja ya kuzuia migogoro, kuimarisha utayari
wa kukabiliana na majanga pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji wa
misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.
Zoezi
la 14 la Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Uamrishaji vya Jumuiya ya
Afrika Mashariki “Ushirikiano Imara 2026” linatarajiwa kuendelea
kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama wa EAC na kuendeleza dira
ya pamoja ya kuwa na Afrika Mashariki yenye amani, usalama na
ustahimilivu mkubwa dhidi ya changamoto mbalimbali
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...