Na Mwandishi Wetu, Pwani
MPANGO wa Rafiki wa Binti umezindua wimbo maalumu wa kielimu wa Afya ya Hedhi ikiwa ni kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Hedhi Mei 28, 2026.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Saumu Zidadu, ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Rafiki wa Binti, amesema pia wamepanua kuongeza usambazaji wa chupi maalumu za hedhi zinazoweza kutumika tena Tanzania.
“Katika kuadhimisha Siku ya Afya ya Hedhi tarehe 28 Mei, Rafiki wa Binti imetoa wimbo mpya wa kielimu wa uhuishaji unaolenga kuwapa wanafunzi wa kike elimu kuhusu afya ya hedhi pamoja na kuhamasisha kujiamini, heshima na mahudhurio shuleni.
“Wimbo huo umeimbwa na kuandikwa na mwimbaji maarufu wa Tanzania Ashura Kitenge, na ni sehemu ya mpango mpana wa elimu ya afya ya hedhi wa Rafiki wa Binti, ambao huwafundisha wasichana namna sahihi ya kutumia, kufua na kutunza chupi maalumu za hedhi zinazoweza kutumika tena suluhisho bunifu na endelevu linalowasaidia wasichana kujisimamia hedhi zao kwa usalama na kujiamini,”imesema taarifa hiyo ya Zidadu.
Kwa upande wake Nancy Bondo, ambaye ni Mkurugenzi wa Rafiki wa Binti, amesema chupi maalumu za hedhi zinazoweza kutumika tena, ni suluhisho jipya na la kipekee katika jamii nyingi za Tanzania na zimekuwa sehemu muhimu ya kazi ya Rafiki wa Binti katika kusaidia wasichana kuendelea na masomo yao na kupunguza unyanyapaa unaohusiana na hedhi.
“Kupitia mpango wake wa Pakiti za Binti, Rafiki wa Binti tayari imetoa zaidi ya jozi 24,000 za chupi maalumu za hedhi zinazoweza kutumika tena kwa wanafunzi wa kike katika maeneo ya Mafinga, Kilwa Masoko, Mkoa wa Kagera na Zanzibar. Chupi hizo zinaweza kutumika tena kwa miaka miwili au zaidi,” amesema na kuongeza:
Kila Pakiti ya Binti ina jozi sita za chupi maalum za hedhi zinazoweza kutumika tena, elimu ya afya ya hedhi, mifuko ya kuhifadhia vifaa vilivyo vikavu na vyenye unyevunyevu
“Jozi nyingine 24,000 za chupi zinatarajiwa kusambazwa katika utekelezaji wa programu zijazo ndani ya miezi michache ijayo wakati taasisi hiyo ikiendelea kupanua huduma zake kote nchini Tanzania. Afya ya hedhi inahusu elimu na fursa,” amesema Nancy Bondo.
Amesema mrejesho kutoka serikalini, kwa walimu na wanafunzi kuhusu Mradi wa Binti umekuwa mazuri sana na unawasaidia wasichana kuendelea kuhudhuria shule wakati wa hedhi zao kwa heshima na kujiamini.
"Rafiki wa Binti inajivunia kuwa mshirika rasmi wa Siku ya Afya ya Hedhi na mwanachama wa Muungano wa Afya ya Hedhi Tanzania, ikifanya kazi pamoja na Serikali na wadau mbalimbali nchini kuboresha uelewa na upatikanaji wa huduma za afya ya hedhi,” amesema.
Amesema Rafiki wa Binti ni mpango unaolenga Tanzania, unaosaidia wasichana kupitia elimu ya afya ya hedhi na utoaji wa chupi maalum za hedhi zinazoweza kutumika tena ili kuwasaidia wasichana kubaki shuleni, kuwa na nguvu na kujiamini.
Amesema Rafiki wa Binti ni programu ya Rafiki Australia Tanzania, taasisi inayoendeshwa kwa kujitolea kwa asilimia 100 na iliyosajiliwa Australia na Tanzania.


.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...