Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewataka Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika taasisi za umma kuhakikisha wanashiriki wenyewe katika kikao kazi cha kitaifa kitakachofanyika jijini Dodoma kuanzia Juni 1 hadi 3, 2026, bila kukosekana wala kutuma wawakilishi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Juma Mkomi amesema kikao hicho ni muhimu katika kuimarisha ufanisi wa utendaji wa rasilimaliwatu serikalini, hivyo kinahitaji ushiriki wa moja kwa moja wa viongozi wote husika.

Amesema kikao hicho kitawakutanisha Wakurugenzi na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara mbalimbali, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuongeza uwajibikaji, ufanisi na nidhamu ya utendaji katika Utumishi wa Umma.

Mkomi amesema kikao hicho kitafanyika katika Ukumbi wa Mabele Hall jijini Dodoma chini ya kaulimbiu isemayo:

“Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Ulio Sikivu, Jumuishi, wenye Matokeo na Uwajibikaji Kuelekea Dira 2050.”

Amefafanua kuwa moja ya ajenda kuu zitakazojadiliwa ni matumizi ya mifumo ya kidijiti katika usimamizi wa rasilimaliwatu, ikiwemo mifumo ya e-Uhamisho, e-Watumishi, e-Utendaji, e-Mrejesho pamoja na HR Assessment, ambayo inalenga kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika taasisi za umma.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mifumo hiyo ya kidijiti ni sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea serikalini ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia pamoja na kutimiza vipaumbele vya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.

Aidha, amesisitiza kuwa viongozi wote watakaohudhuria watapatiwa maelekezo mahsusi kuhusu usimamizi bora wa rasilimaliwatu serikalini, huku akibainisha kuwa hakutakuwa na nafasi ya uwakilishi, kutokana na umuhimu na uzito wa maudhui yatakayojadiliwa katika kikao hicho.

“Ni muhimu kila kiongozi anayehusika kuhudhuria mwenyewe ili kupata uelewa wa moja kwa moja na maelekezo ya kimkakati kuhusu maboresho ya sekta ya rasilimaliwatu,” ameweka msisitizo Mkomi.

Vilevile, kikao hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete, ambaye anatarajiwa kutoa mwelekeo wa serikali kuhusu maboresho ya utumishi wa umma na usimamizi wa rasilimaliwatu nchini.

Serikali imesema kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utawala bora, kuongeza uwajibikaji wa watumishi wa umma na kuhakikisha taasisi za serikali zinaendeshwa kwa ufanisi unaozingatia matokeo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...