Na Janeth Raphael MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Magereza kufanya tafiti za kina zitakazowezesha kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kuwasaidia wafungwa wenye ujuzi wanaporejea uraiani, ili waweze kujitegemea kiuchumi na kuepuka kurejea katika makosa ya uhalifu.
Rais Samia amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuimarisha mfumo wa urekebishaji nchini kwa kuhakikisha wafungwa wanaopata mafunzo ya ufundi na stadi mbalimbali wakiwa magerezani wanapata mazingira rafiki ya kuanza maisha mapya baada ya kutumikia vifungo vyao.
Ametoa maelekezo hayo leo Mei 9, 2026, wakati akihutubia hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi Na. 28 pamoja na Uongozi Daraja la Pili Kozi Na. 48 iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), Ukonga jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema wafungwa wengi wamekuwa wakipata ujuzi muhimu wakiwa magerezani kupitia mafunzo mbalimbali ya ufundi stadi, ushonaji, kilimo, useremala na shughuli nyingine za uzalishaji, lakini changamoto kubwa imekuwa ni ukosefu wa mtaji au mifumo ya kuwawezesha kuanza maisha mapya wanapotoka gerezani.
Amesema kuanzishwa kwa mfuko huo kutasaidia kuwapa nguvu ya kuanza upya kwa kutumia maarifa na taaluma walizozipata, jambo litakalosaidia kupunguza matukio ya kurudia makosa pamoja na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Tunapaswa kuwapa nafasi ya pili ya maisha. Kama wamejifunza kazi na stadi mbalimbali wakiwa magerezani, basi wanapotoka wanahitaji kuungwa mkono ili waweze kujitegemea na kuwa sehemu ya maendeleo ya nchi,” alisisitiza Rais Samia.
Aidha, amemuelekeza Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania, Jeremiah Katungu kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tafiti za sera na mifumo bora itakayowezesha utekelezaji wa mpango huo kwa ufanisi.
Rais Samia pia alipongeza Jeshi la Magereza kwa kuendelea kuboresha mfumo wa urekebishaji wa wafungwa kwa kuwapatia elimu, maadili na stadi za maisha zinazowaandaa kuwa raia wema baada ya kumaliza vifungo vyao.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, maafisa wa Jeshi la Magereza pamoja na washiriki wa mafunzo waliohitimu kozi hizo za uongozi.


































Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...