
*Uwezo wa Bandari ya Dar kuongezeka maradufu ifikapo 2030
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeanza mikakati ya kupunguza msongamano wa makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza ufanisi wa Bandari Kavu nchini.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, wakati wa kikao cha wadau wa mamlaka mbalimbali za Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Salum alisema lengo la kikao hicho ni kujadili namna ya kuanzisha na kuendeleza bandari kavu kwa kufuata taratibu na sheria, pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto ya foleni ya magari katika jiji hilo.
Alieleza kuwa changamoto zilizopo ni pamoja na msongamano wa magari barabarani, ucheleweshaji wa upatikanaji wa mizigo kwa wateja, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji, pamoja na uwezo mdogo wa baadhi ya bandari kavu kushindwa kuhudumia mizigo mingi.
Kwa mujibu wa TASAC, Bandari ya Dar es Salaam inapokea wastani wa makontena 110,000 kwa mwezi, ambapo asilimia 45 ya makontena hayo husafirishwa kwenda nchi jirani zinazotumia bandari hiyo ikiwemo Zambia, Malawi,Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) , Rwanda pamoja na Burundi.
Alisema uwezo wa sasa wa Bandari ya Dar es Salaam ni kuhudumia makontena 28,000 kwa wakati mmoja, huku kitaalamu kiwango cha matumizi kisichopaswa kuzidi asilimia 65 ili kuhakikisha ufanisi wa huduma unaendelea kuwa mzuri.
“Bandari si sehemu ya kuhifadhi makontena bali ni eneo la kupokelea na kusafirisha mizigo. Ndiyo maana uwepo wa bandari kavu ni muhimu katika kusaidia shughuli hizo,” alisema Salum.
Aidha, alisema uwezo wa bandari kavu zilizopo kwa sasa jijini Dar es Salaam hauwezi kuhifadhi zaidi ya makontena 37,000, hali inayosababisha changamoto kubwa kutokana na ongezeko la mizigo inayoingia na kutoka nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Usafiri Majini, Nelson Mlali, alisema zaidi ya asilimia 80 ya bandari kavu nchini zipo Dar es Salaam kutokana na mahitaji makubwa ya soko na uwepo wa viwanda vingi.
Mlali alisema Wilaya ya Temeke inaongoza kwa kuwa na bandari kavu 74 sawa na asilimia 64.3, ikifuatiwa na Ilala yenye bandari kavu 22, Kigamboni bandari kavu 13, Kinondoni nne na Ubungo mbili.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri wa Majini kutoka Wizara ya Uchukuzi, Mussa Shashula, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari kavu ili kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema matokeo ya uwekezaji huo yameanza kuonekana baada ya kiwango cha mizigo bandarini kuongezeka kutoka tani milioni 18 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 32 mwaka 2024/25.


.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...