Na Janeth Raphael MichuziTv .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kali kwa viongozi wapya walioapishwa, akisisitiza kuwa madaraka waliyopewa si ya kujinufaisha wala kujiona bora, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na uwajibikaji.
Akizungumza leo katika hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia aliwakumbusha viongozi hao kuwa nafasi walizonazo ni za muda na zinapaswa kutumika kwa manufaa ya umma, si kwa maslahi binafsi.
Amesisitiza umuhimu wa unyenyekevu kwa viongozi, akieleza kuwa ni kosa kubwa kwa yeyote kujivuna au kujiona hawezi kuwajibishwa kwa sababu ya cheo chake. “Madaraka ni dhamana nzito mbele ya Mungu na jamii, hivyo kila kiongozi anapaswa kuyaheshimu na kuyatumia kwa haki,” alionya.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia pia ameeleza sababu za kumteua Eveline Munisi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, licha ya kuwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi. Alifafanua kuwa uamuzi huo umetokana na sifa, uzoefu na uwezo aliouona katika wasifu wake wa kitaaluma, akiamini kuwa ana mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa Serikali.
Aidha, Rais Samia alirejea falsafa ya James Mbatia, aliyewahi kusisitiza umuhimu wa “kumhudumia Mama Tanzania,” akisema kauli hiyo inaendelea kuwa chachu ya kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao za kisiasa, kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya Taifa.
Akizungumzia ajira, Rais Samia alibainisha kuwa Serikali inaendelea kupanua fursa kwa vijana ndani na nje ya nchi. Alieleza kuwa zaidi ya vijana 7,000 tayari wamepata nafasi za ajira nje ya nchi mwaka huu, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda haki na stahili zao wanapokuwa kazini.
Pia aligusia umuhimu wa kuimarisha mahusiano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi, akisema ushirikiano huo ni msingi wa kudumisha amani mahali pa kazi na kuchochea maendeleo endelevu ya nchi.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia aliwataka viongozi wote walioapishwa kusimamia majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kujituma, ili kuendana na matarajio ya Watanzania na kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa lenye ustawi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...