Wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutumia kikamilifu fursa ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ili kupata huduma muhimu za kisheria na vyeti kwa wakati, badala ya kusubiri hadi wanapokumbana na changamoto zinazohitaji nyaraka hizo.
Wito huo umetolewa huku kukisisitizwa kuwa uwepo wa wataalamu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) katika kampeni hiyo ni nafasi adhimu ya kupata ushauri na msaada wa moja kwa moja kuhusu masuala ya Wosia, Ndoa, Talaka, vyeti na mirathi.
Akizungumza Mei 2, 2026, Afisa Msajili Mwandamizi kutoka RITA Dodoma, Mwinyijuma Maneno Moshi, ametoa rai hiyo na kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la taasisi hiyo katika maadhimisho ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria yanayoendelea mkoani Dodoma.
Kampeni hiyo, inayoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria, inaendelea kwa muda wa siku 15 kuanzia Mei 1, 2026, na inafanyika katika viwanja vya Mtekelezo vilivyopo jijini Dodoma.
Moshi amesema kuwa ndani ya kipindi hicho, RITA inatoa huduma mbalimbali ikiwemo usajili mpya wa vyeti vya kuzaliwa, kubadilisha vyeti vya zamani, pamoja na uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa ambapo mwananchi ataweza kupata cheti chake ndani ya masaa machache.
Aidha, huduma nyingine zinazotolewa ni pamoja na utoaji wa vyeti vya vifo, vyeti vya ndoa pamoja na talaka, lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa nyaraka muhimu kwa wananchi.
Mbali na hilo, Moshi amewahimiza Watanzania kutembelea banda la RITA ili kupata elimu kuhusu umuhimu wa kuandika wosia, ameeleza kuwa wosia husaidia katika mgawanyo wa mali pindi mtu anapofariki, ambapo mmoja wa mashahidi atatakiwa kutoa taarifa RITA na kufuatiwa na taratibu za kuwasilisha wosia katika sehemu husika.
Ametaja faida za kuandika na kuhifadhi wosia RITA kuwa ni pamoja na taasisi hiyo kuwa ya serikali isiyo na ukomo wa maisha, kuwa na wataalamu wa sheria waliobobea katika masuala ya mirathi, uwepo wa sehemu salama ya kuhifadhi wosia pamoja na gharama nafuu za huduma hiyo.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...