WANANCHI wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Kitulo mkoani Njombe wameendelea kunufaika kiuchumi kupitia ongezeko la matukio ya utalii wa michezo, huku mbio za Kitulo Garden Marathon zikionekana kuwa kichocheo kipya cha ajira na biashara ndogo ndogo katika maeneo hayo.
Katika tukio hilo lililofanyika Mei 2, 2026, wakazi wa Wilaya ya Makete na maeneo ya jirani walijitokeza kwa wingi kuuza bidhaa na kutoa huduma mbalimbali kwa washiriki na wageni, hatua iliyosaidia kuongeza kipato cha kaya na kupunguza utegemezi wa shughuli hatarishi kama ujangili.
Akizungumza wakati wa mbio hizo, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, alisema kuwa utalii wa michezo umeendelea kuwa daraja muhimu la kuwaunganisha wananchi na fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za asili.
Alieleza kuwa kupitia huduma za malazi, chakula, usafiri na uuzaji wa bidhaa za mikono, wananchi wengi wameweza kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao, huku akisisitiza kuwa sekta ya utalii ni jumuishi na inagusa watu wa kada mbalimbali.
Mbali na faida za kiuchumi, marathon hiyo pia imechangia maendeleo ya kijamii baada ya kompyuta 40 kutolewa kwa shule nane za sekondari wilayani Makete, hatua inayolenga kuinua kiwango cha elimu kwa vijana wa eneo hilo.
Kwa upande wa uhifadhi, viongozi wa TANAPA wamesema matukio kama hayo yanaongeza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda hifadhi, kwani yanawaonesha moja kwa moja manufaa ya kiuchumi yanayotokana na rasilimali hizo.
Kitulo Garden Marathon, iliyojumuisha mbio za kilomita 5, 10 na 21, imeendelea kujijengea umaarufu kama jukwaa la kukuza afya, kutangaza vivutio vya utalii na kuimarisha uchumi wa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.






.jpeg)
.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...