Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

RAIS wa Kenya William Ruto amesema ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Kenya utakuwa chachu ya kukuza uchumi na kupanua fursa za ajira kwa wananchi wa mataifa hayo mawili, hususan vijana.

Ruto ametoa kauli hiyo akisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa pamoja katika miradi ya kimkakati, ikiwemo mpango wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta mkoani Tanga.

Amesema serikali ya Kenya, pamoja na nchi nyingine ikiwemo Uganda, iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo, ambao utafungua milango ya biashara na kukuza viwanda katika ukanda huo.

“Watu wa Tanzania, nyinyi ni wenye bahati kwamba tunajadili namna ya kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta huko Tanga. Serikali ya Kenya iko tayari kufanya hilo, na pia Uganda iko tayari. Hii ni fursa ya pamoja ya kujenga mfumo wa amani wa biashara na viwanda hapa hapa Tanga,” amesema Ruto.

Aidha, ameeleza kuwa ukaribu wa kijiografia kati ya Tanga na Mombasa, ambao ni takribani kilomita 190, pamoja na uwepo wa miundombinu ya bomba la mafuta kutoka Mombasa, utarahisisha utekelezaji wa mradi huo na kuimarisha biashara ya kikanda.

Mbali na sekta ya mafuta, Rais Ruto ameibainisha kuwa kuna fursa pia katika uchakataji wa madini, akisisitiza kuwa wakati umefika kwa nchi za Afrika Mashariki kuacha kuuza malighafi nje bila kuongeza thamani.

“Tunapaswa kuacha kuuza nje malighafi. Kwa kufanya hivyo tunauza nje ajira, fursa na utajiri wetu. Badala yake, tunahitaji kuchakata rasilimali zetu hapa hapa ili kuongeza thamani na kujenga uchumi imara na endelevu,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa mazungumzo yake na Rais wa Tanzania yamelenga kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi wa eneo hili, akibainisha kuwa huo ndio mwelekeo sahihi wa maendeleo ya kiuchumi kwa sasa.

Kauli ya Ruto inaakisi dhamira ya nchi za Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupunguza utegemezi wa kuuza malighafi, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza viwanda na kuimarisha uchumi wa kikanda.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...