▪️︎ Dkt. Mwigulu asema Serikali imejipanga kujenga jengo lenye hadhi ya kimataifa

▪️︎ Asema Mwanza itaendelea kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi Kanda ya Ziwa


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha Uwanja wa Ndege wa Mwanza unaboreshwa na kujengwa katika hadhi ya kimataifa ili kuendana na hadhi ya jiji la Mwanza kama kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi Kanda ya Ziwa.

Amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akitoa kauli ya Serikali kuhusu hoja ya maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza iliyowasilishwa na Mbunge wa Magu, Mhe. Boniventura Kiswaga, katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwenye Kikao cha 28 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 13, leo Mei 13, 2026.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza na imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa pamoja na kukidhi viwango vya kimataifa.

“Zipo jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika kuhakikisha kwamba uwanja wa ndege wa Mwanza unaendana na hadhi ya Mwanza kama kitovu cha shughuli za kiuchumi Kanda ya Ziwa,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na mazungumzo ya kuongeza eneo la uwanja huo ili kuwezesha upanuzi wa njia ya kurukia ndege (runway) pamoja na maboresho mengine muhimu ya miundombinu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imekubaliana kujenga jengo jipya la abiria litakalokuwa na hadhi ya kimataifa na kuendana na mahitaji ya muda mrefu ya uwanja huo.

“Imekuja kukubalika kwamba tujenge jengo ambalo halitahitaji kubomolewa tena baada ya muda mfupi, bali jengo lenye hadhi na viwango vya viwanja vya ndege vya kimataifa,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea na mpango huo sambamba na utekelezaji wa miradi mingine ya viwanja vya ndege nchini, huku akisisitiza kuwa dhamira ya kuifanya Mwanza kuwa kitovu kikubwa cha uchumi kupitia usafiri wa anga ipo pale pale.

Waziri Mkuu amesema Serikali itafanya kikao maalumu na wabunge wa Mkoa wa Mwanza pamoja na wizara husika ili kuondoa changamoto zilizokuwa zikikwamisha utekelezaji wa mradi huo na kuruhusu hatua zinazofuata kuendelea.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...