Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni Dodoma
-Serikali Yaeleza hatua Zinazoimarisha Ajira na Mazingira ya Kazi kwa Watumishi Wenye Ulemavu
Serikali imesema inaendelea kuimarisha utekelezaji wa sera, sheria na miongozo inayolenga kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa za ajira pamoja na mazingira rafiki ya kazi ndani ya Utumishi wa Umma na sekta binafsi nchini.
Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Lowassa Qwaray wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa Alex ambaye alihoji hatua iliyofikiwa na Serikali katika kutekeleza Mwongozo wa Ajira na Mazingira ya Kazi kwa Watumishi wenye Ulemavu katika taasisi za umma.
Akijibu swali hilo, Qwaray amesema Serikali imeweka msingi wa kisheria na kisera kupitia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la mwaka 2008 pamoja na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura ya 183, ambazo zimeweka masharti mahsusi kuhusu ajira, haki za kazi na mazingira rafiki kwa watumishi wenye ulemavu katika Utumishi wa Umma na sekta binafsi.
Amesema katika kuhakikisha masharti hayo yanatekelezwa kwa vitendo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika maeneo ya kazi, ikiwemo kutungwa kwa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 pamoja na Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma za mwaka 2021.
Aidha, Serikali imeandaa Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu wa mwaka 2008 ambao unalenga kusaidia taasisi za umma kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa watumishi wenye ulemavu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi sawa na watumishi wengine.
Qwaray amesema miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu fikivu katika maeneo ya kazi, huduma zinazozingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa taasisi mbalimbali kuhusu umuhimu wa usawa na ujumuishwaji mahali pa kazi.
“Serikali itaendelea kuweka misingi thabiti ya utekelezaji wa sera, sheria na miongozo kuhusu watumishi wenye ulemavu kwa kutoa elimu, kuhamasisha na kusimamia ujenzi wa miundombinu fikivu na rafiki kwa watu wenye ulemavu katika Utumishi wa Umma,” amesema Qwaray.
Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama, jumuishi na yanayomwezesha kila mtumishi kutekeleza wajibu wake bila vikwazo vinavyotokana na hali ya ulemavu.
Hatua hizo zinaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha usawa wa kijamii, kuongeza fursa za ajira kwa watu wenye ulemavu na kuhakikisha haki zao zinazingatiwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ndani ya taasisi za umma nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...