Kampuni ya huduma za kidijitali na mawasiliano, Yas, kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara wa Ufaransa Tanzania (French Tanzania Chamber of Commerce), imezindua programu ya “Startups za Viwango”, mpango unaolenga kukuza kampuni changa za ubunifu nchini kupitia mafunzo, ushauri wa kitaalamu, fursa za uwekezaji pamoja na kuimarisha biashara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton-Bacara, alisema mpango huo unalenga kusaidia vijana wabunifu kubadilisha mawazo yao kuwa biashara endelevu na zenye ushindani.
Alisema licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya vijana wenye ubunifu na mawazo yenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko, kampuni nyingi changa bado zinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa ujuzi wa biashara, ufadhili na mwongozo wa kitaalamu.
“Kuna vijana wengi nchini wenye mawazo mazuri na suluhisho kwa jamii, lakini wengi wao hukosa mazingira sahihi ya kuyaendeleza na kuyakuza. Kupitia ‘Startups za Viwango’, tunataka kusaidia kuziba pengo hilo na kuwawezesha kufikia hatua kubwa zaidi,” alisema Canton-Bacara.
Aliongeza kuwa Yas inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali ili kuweka mazingira bora ya ukuaji wa biashara na ubunifu nchini.
“Ubunifu hauhitaji mtandao pekee, bali unahitaji mazingira yanayowezesha biashara kukua, kupata ushauri na kufikia masoko mapya. Ushirikiano huu unaonesha dhamira yetu ya kusaidia uchumi wa ubunifu nchini,” aliongeza.
Kupitia programu hiyo, kampuni changa zitapata mafunzo ya biashara, ushauri kutoka kwa wataalamu, nafasi za kukutana na wawekezaji pamoja na fursa za kuunganishwa na masoko ya kimataifa.
Sehemu ya programu hiyo ni pamoja na Yas Masterclass itakayotekelezwa kwa kushirikiana na Yas Business, ambapo wataalamu wa kampuni hiyo watashirikiana na waanzilishi wa startups kuimarisha mifumo yao ya biashara, mikakati ya ukuaji na uwezo wa kuvutia uwekezaji.
“Tunawaamini vijana wa Tanzania na tunaamini biashara wanazojenga zina uwezo wa kuzalisha ajira, kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ubunifu barani Afrika,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Ufaransa Tanzania, Bi. Hannah De Somviele, alisema ushirikiano huo una lengo la kuimarisha mazingira ya ubunifu nchini na kuzisaidia ‘startups’ za Tanzania kupata nafasi katika masoko ya kimataifa.
“Tunaamini wajasiriamali wa Tanzania wana uwezo mkubwa wa kushindana kimataifa. Kupitia programu hii, tunataka kuwapatia mitandao, mwongozo na fursa zitakazowawezesha kukuza biashara zao kwa kiwango cha kimataifa,” alisema De Somviele.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...