Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni Dodoma.
Serikali imeendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana nchini kwa kuanzisha na kusimamia programu mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu na vijana wengine ili waweze kuajirika au kujiajiri.
Hatua hizo zimeelezwa bungeni na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Eveline Munisi, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Amina Ali Mzee, aliyehoji hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wanaomaliza masomo yao.
Dkt. Munisi amesema Serikali imeandaa Mwongozo wa Taifa wa Mafunzo ya Uzoefu Kazini wa mwaka 2017, unaolenga kuratibu utoaji wa mafunzo kwa vitendo kwa kushirikisha sekta ya umma na binafsi ili kuwapa vijana nafasi ya kupata uzoefu wa kazi kabla ya kuingia rasmi kwenye soko la ajira.
Amesema kupitia mwongozo huo pamoja na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, vijana wengi wamepata mafunzo ya vitendo yanayowawezesha kuongeza ushindani katika soko la ajira.
Kwa mujibu wa Dkt. Munisi, jumla ya wahitimu 32,194 tayari wamenufaika na mafunzo hayo kwa kupata ujuzi wa kazi, maadili ya utumishi pamoja na uzoefu unaowasaidia kuajiriwa katika taasisi mbalimbali au kujiajiri katika maeneo yao.
Aidha, Serikali imeendelea kuanzisha programu maalum zinazowalenga vijana katika sekta zinazozalisha ajira kwa wingi ikiwemo kilimo kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT), sekta ya madini kupitia MBT pamoja na sekta ya uvuvi kupitia BBT-LIFE.
Dkt. Munisi amesema lengo la programu hizo ni kuwawezesha vijana kutumia fursa zilizopo katika rasilimali za nchi kwa kujenga uwezo wa uzalishaji, ubunifu na ujasiriamali ili waweze kujitegemea kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kufungua fursa za ajira nje ya nchi kwa kuwaunganisha Watanzania na waajiri wa kimataifa kupitia mikataba ya ushirikiano na mataifa mbalimbali ikiwemo Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na Iran.
Amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, jumla ya vijana 7,593 wamefanikiwa kupata ajira nje ya nchi kupitia mpango huo katika fani tofauti tofauti.
Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha mazingira ya ajira na uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata fursa za ajira na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa taifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...