Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni Dodoma
Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, amempongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Alban Kihulla, kwa utendaji wake wa kazi wenye weledi na ushirikiano mzuri katika kutekeleza majukumu ya taasisi hiyo.
Shabiby amesema WMA imekuwa ikitoa ushirikiano wa karibu kila inapohitajika, hali ambayo imechangia kuimarisha usimamizi wa vipimo na kulinda maslahi ya wananchi pamoja na wafanyabiashara nchini.
Mbunge huyo ametoa pongezi hizo leo Mei 22, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Pamoja na pongezi hizo, Shabiby ameishauri WMA kuongeza umakini katika kudhibiti ubora wa nondo zinazozalishwa na baadhi ya viwanda nchini, akieleza kuwa bado kuna changamoto ya uzalishaji wa nondo zisizokuwa na ujazo na viwango sahihi, jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa majengo yanayojengwa kwa kutumia bidhaa hizo.
Amesema baadhi ya viwanda vinavyomilikiwa na wawekezaji wa kigeni vinaendelea kuzalisha bidhaa zenye viwango hafifu huku vikifanya biashara kama kawaida, hali inayohitaji hatua kali zaidi kutoka kwa mamlaka husika.
“Tusibaki kwenye kutoa faini pekee. Viwanda vinavyotengeneza nondo zisizokidhi viwango vinapaswa kufungiwa ili kulinda usalama wa wananchi na ubora wa ujenzi nchini,” amesema Shabiby.
Aidha, amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa viwango vya bidhaa za ujenzi ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya viwanda pamoja na kulinda maisha na mali za Watanzania.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...