Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni Dodoma .

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeweka mikakati kabambe ya kuimarisha utendaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza ufanisi wa biashara ya mazao na kuhakikisha ubora wa bidhaa zinazohifadhiwa nchini.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara bungeni, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema WRRB imejipanga kuboresha usimamizi wa mfumo huo ili uweze kufanya kazi kwa viwango vya juu zaidi na kuwanufaisha wakulima pamoja na wafanyabiashara.

Amesema miongoni mwa hatua zitakazotekelezwa ni kuimarisha udhibiti wa ubora wa mazao yanayoingia na kutoka kwenye maghala yaliyo chini ya mfumo huo, sambamba na kuongeza ufuatiliaji kwa waendesha maghala, wakaguzi na mameneja dhamana ili kuhakikisha uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria na kanuni zilizowekwa.

Aidha, WRRB itaendelea kutoa elimu kwa umma na kufanya kampeni za uhamasishaji kuhusu matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, hatua inayolenga kuongeza uelewa kwa wakulima na wafanyabiashara kuhusu faida za mfumo huo katika uhifadhi salama na uuzaji wa mazao kwa tija zaidi.

“WRRB imejipanga kuendeleza kampeni za elimu kwa umma na kuongeza uhamasishaji kuhusu matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuongeza ushiriki wa wadau mbalimbali,” amesema Kapinga.

Katika hatua nyingine, Bodi hiyo inaendelea na mchakato wa kupata cheti cha ithibati ya ubora wa kimataifa (ISO), hatua inayotarajiwa kuongeza uaminifu wa mfumo huo ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Serikali inaamini kuwa maboresho hayo yatachangia kuongeza thamani ya mazao ya wakulima, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuongeza mapato kwa wananchi pamoja na kukuza uchumi wa taifa.

WRRB imeeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuifanya sekta ya kilimo kuwa na tija kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa ya uhifadhi, usimamizi na biashara ya mazao nchini.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...