KATIKA maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, wito umetolewa kwa familia za Tanzania kuzingatia uzazi wa mpango kama njia muhimu ya kujenga familia imara, kukuza uchumi na kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yatakayowawezesha kufikia ndoto zao.

Imeelezwa kuwa familia ndiyo taasisi ya msingi katika ujenzi wa taifa, uchumi na maendeleo ya nchi yoyote duniani, lakini changamoto ya ongezeko kubwa la watu imeendelea kuwa kikwazo kwa familia nyingi kumudu gharama za malezi, elimu na afya kwa watoto.

Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ina ongezeko la watu linalozidi asilimia tatu kwa mwaka, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko wastani wa Bara la Afrika wa asilimia mbili na wastani wa dunia wa asilimia moja. Hali hiyo imeelezwa kuongeza mzigo wa utoaji wa huduma za kijamii huku taifa likikabiliwa na changamoto ya kujenga rasilimali watu yenye ubora.

Kwa mujibu wa tathmini ya maendeleo ya uchumi, Tanzania kwa sasa ipo nafasi ya 81 kwa ukubwa wa uchumi duniani na ya 165 kwa pato la mtu mmoja, huku ikiwa nafasi ya 20 kwa idadi ya watu duniani. Makadirio yanaonesha kuwa ifikapo mwaka 2050, idadi ya watu inaweza kufikia takribani milioni 137, jambo litakalohitaji uwekezaji mkubwa katika elimu, afya na ajira ili kuhakikisha wananchi wanapata maisha bora.

Aidha, imeelezwa kuwa nchi kama China zilipata mafanikio ya haraka ya kiuchumi kutokana na sera za kudhibiti ongezeko la watu, huku India ikiwa na changamoto ya pato la mtu mmoja licha ya kuwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani. Hali hiyo imeelezwa kuwa somo kwa Tanzania katika kupanga ukuaji wa uchumi unaokwenda sambamba na ukuaji wa watu.

Wadau wa maendeleo wameeleza kuwa ili Tanzania ifikie malengo ya maendeleo ya muda mrefu, kuna haja ya kujenga familia zenye watoto wachache lakini wenye afya, maadili, elimu na maarifa yatakayowawezesha kushindana katika soko la dunia. Pia imesisitizwa kuwa uwekezaji katika sekta za elimu na afya hauwezi kutegemea kodi na mikopo pekee, bali unahitaji ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP) ili kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa nguvu kazi yenye tija kwa taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...