Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma .

Shughuli za Bunge jijini Dodoma zilisimama kwa muda leo Alhamisi Mei 14, 2026 baada ya kutokea hitilafu ya mfumo wa sauti ndani ya ukumbi mkuu wa Bunge, hali iliyomlazimu Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu kuahirisha kikao hicho kwa muda.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 2:59 asubuhi wakati Spika akiingia ukumbini akiwa ameongozana na timu ya makatibu wa Bunge pamoja na wapambe wa Bunge waliokuwa wakiongozwa na mbeba Siwa. Licha ya vipaza sauti kuonekana kuwaka ukumbi mzima, hakukuwa na sauti yoyote iliyokuwa ikisikika.

Hitilafu hiyo ilianza kubainika mara baada ya sauti ya mpambe anayebeba Siwa kushindwa kusikika wakati akiashiria kuwasili kwa kiongozi wa Bunge, huku akionekana akizungumza bila sauti kufika kwa wabunge na wageni waliokuwapo ukumbini.

Baada ya Spika kusimama tayari kwa ajili ya kusoma dua ya kuanza kikao, sauti yake nayo haikusikika, jambo lililosababisha taharuki ya muda mfupi ndani ya ukumbi huo. Dakika chache baadaye, mmoja wa wapambe aliingia na kuondoa Siwa kutoka sehemu yake ya kawaida kabla ya kuihifadhi kwenye droo ya meza ya mbele.

Muda mfupi baada ya hali hiyo, Spika Zungu aliondoka kwenye kiti chake huku Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba naye akisimama na kuondoka ukumbini.

Baadaye wapambe wa Bunge walionekana wakilibeba Siwa ndani ya sanduku maalumu na kutoka nalo nje ya ukumbi, huku mfumo wa vipaza sauti ukiendelea kuonyesha mwanga wa kuwaka lakini bila kutoa sauti yoyote.

Tukio hilo limejiri siku moja tu baada ya kusikika kwa mlio wa king’ora ndani ya ukumbi wa Bunge uliozua taharuki miongoni mwa wabunge kabla ya Mwenyekiti wa Bunge, Deo Mwanyika kueleza kuwa hakukuwa na hatari yoyote na shughuli za Bunge kuendelea kama kawaida.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana ndani ya Bunge, kikao hicho kinatarajiwa kuendelea baadaye katika Ukumbi wa Pius Msekwa wakati mafundi wakiendelea kushughulikia hitilafu iliyojitokeza kwenye mfumo wa sauti wa ukumbi mkuu.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...