Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Wakati Tanzania ikiendelea kukabiliwa na changamoto ya ongezeko la taka ngumu mijini na vijijini, Serikali imezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha mapato yatokanayo na shughuli za usafi na udhibiti wa taka yanatumika moja kwa moja kuboresha huduma hizo pamoja na kuimarisha mazingira.

Hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na usimamizi wa taka huku Serikali ikihimiza jamii kuanza kuzitazama taka kama rasilimali yenye thamani ya kiuchumi badala ya mzigo wa mazingira.

Akizungumza leo Mei 12, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Afua za Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Miji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe amesema halmashauri zote zinapaswa kutenga na kurejesha asilimia 10 ya mapato yanayotokana na shughuli za udhibiti wa taka ili kuviwezesha vitengo vya usafi wa mazingira kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo “Taka Ngumu ni Mali; Tumia, Rejeleza na Weka Miji Safi.”

Profesa Shemdoe amesema bado hali ya usimamizi wa taka nchini si ya kuridhisha kutokana na baadhi ya halmashauri kushindwa kuwa na maeneo rasmi ya kutupia taka.

Amesema kati ya halmashauri 184 zilizopo nchini, ni halmashauri 43 pekee zenye madampo rasmi, jambo ambalo linaathiri juhudi za usafi wa mazingira na kuongeza hatari ya uchafuzi wa mazingira pamoja na magonjwa ya mlipuko.

“Ni muhimu kuhakikisha taka zinakusanywa na kuhifadhiwa katika maeneo maalum ili kulinda afya za wananchi na kuweka mazingira safi katika miji na makazi yetu,” amesema.

Aidha, ameonya kuhusu tabia ya utupaji holela wa taka kwenye mitaro ya maji, akisema hali hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha mafuriko wakati wa mvua kutokana na kuziba kwa mifumo ya maji.

Kwa mujibu wa Profesa Shemdoe, viongozi wa mikoa, wilaya pamoja na serikali za mitaa wanapaswa kuhakikisha suala la usafi wa mazingira linakuwa agenda ya kudumu katika vikao vya maamuzi ili kuongeza uwajibikaji katika jamii.

Katika hatua nyingine, Serikali imehimiza wananchi kuanza kutenganisha taka kuanzia zinakozalishwa ili kurahisisha shughuli za urejelezaji wa plastiki, vyuma, karatasi na taka nyingine zinazoweza kutumika tena.

Amesema mfumo huo utasaidia kuongeza thamani ya taka na kufungua fursa mpya za ajira na biashara kwa wananchi, hususan vijana na wanawake.

“Tunapaswa kubadili mtazamo kuhusu taka. Zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha kipato kupitia shughuli za ukusanyaji, uchakataji na urejelezaji,” amesema.

Profesa Shemdoe pia amewataka vijana na wanawake kutumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kuanzisha miradi ya ukusanyaji na uchakataji wa taka ngumu ili kujiongezea kipato huku wakichangia uhifadhi wa mazingira.

Amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Japan kutafuta teknolojia za kisasa za uteketezaji na urejelezaji wa taka kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu la usimamizi wa taka nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma umeongeza bajeti ya usafi wa mazingira kutoka Shilingi milioni 750 hadi Shilingi bilioni 3 kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema fedha hizo zitatumika kununua vifaa vya usafi, kuboresha ukusanyaji wa taka pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Mabadiliko ya Tabianchi na Tathmini kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Kanizio Manyika amesema Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni 17 za taka ngumu kila mwaka huku asilimia 60 hadi 75 ya taka hizo zikibaki kwenye mazingira kutokana na kutokusanywa ipasavyo.

Ameonya kuwa hali hiyo ni tishio kwa afya za wananchi na mazingira na kusisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo endelevu ya usimamizi wa taka.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birango amesema takwimu zinaonyesha magonjwa sita kati ya 10 yanayoisumbua jamii yanachangiwa na uchafuzi wa mazingira pamoja na mifumo duni ya usimamizi wa taka.

Awali, Mwenyekiti wa Wakuu wa Vitengo vya Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira Tanzania Bara, William Mpangala aliitaka Serikali kutoa maelekezo madhubuti zaidi kwa halmashauri ili kuhakikisha fedha zinazotokana na shughuli za udhibiti wa taka zinarejeshwa kikamilifu katika kuboresha huduma za usafi wa mazingira.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...