Na Mwandishi Wetu
KUELEKEA msimu mwingine wa Tamasha la Kyela Ibhasa Festival linalofanyika kila mwisho wa mwaka wilayani Kyela mkoani Mbeya, kikundi cha wazawa wa Kyela kiitwacho Bhalondo kimeweka rekodi mpya ya uchangiaji baada ya kufanikisha kukusanya shilingi milioni 2.85 kwa ajili ya maandalizi ya tamasha hilo.
Rekodi hiyo imekuwa ya kipekee tangu kuanzishwa kwa umoja huo, huku kikundi hicho chenye wanachama 19 kikionekana kuwa mfano wa kujitolea na mshikamano katika kuendeleza shughuli za kijamii na maendeleo ya nyumbani kwao.
Kwa mujibu wa wanakikundi hao, mafanikio hayo yametokana na utaratibu waliouweka wa kuchanga fedha kila mwisho wa mwezi kwa lengo la kuhakikisha kabla ya mwezi Juni tayari wanakuwa wamemaliza mchango wao, ili muda unaobaki uwe wa kujipanga zaidi kwa ajili ya kufanikisha tamasha hilo litakalofanyika mwezi Desemba mwaka huu.
Mtunza Hazina wa kikundi hicho, Janeth Mophaty, amesema siri ya mafanikio yao ni moyo wa uzalendo na dhamira ya dhati ya kuipenda Kyela pamoja na kutambua kuwa maendeleo ya tamasha hilo yanahitaji watu kujitoa kwa hali na mali.
“Tumekuwa na ushirikiano mkubwa ndani ya kikundi chetu. Kila mmoja ameonyesha dhamira ya kuona Kyela Ibhasa Festival inakuwa kubwa zaidi mwaka hadi mwaka. Ndiyo maana tumeweza kuvunja rekodi na kumaliza mchango wetu mapema,” amesema Janeth.
Amesema tamasha hilo limeendelea kuwa chachu ya kuwakutanisha wana Kyela waliopo ndani na nje ya nchi, sambamba na kutangaza utamaduni, utalii na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo wilayani humo.
Ikumbukwe kuwa , Umoja wa Kyela Ibhasa Festival umeweka utaratibu wa kila mwana Kyela kuchangia kuanzia shilingi 150,000 na kuendelea, kwa ajili ya kuhakikisha maandalizi ya tamasha hilo yanafanikiwa kama ilivyokusudiwa.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...