Na Mwandishi wetu - Msumbiji
TANZANIA inaandaa Mpango wa Kitaifa wa Hatua za Mapema za kujiandaa, kukabiliana na ukame kwa maeneo yanayokabiliwa na janga hilo kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), ikiwa ni jitihada za kupunguza athari za janga hilo nchini.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya serikali kuachana na utaratibu wa kusubiri madhara yatokee ndipo ichukue hatua, na badala yake kuelekea katika usimamizi wa hatari unaozingatia maandalizi na tahadhari za mapema.
Hayo yameelewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi, katika ziara ya kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Msumbiji kuhusu hatua za mapema kabla ya majanga unaoendelea kwa siku tano kuanzia tarehe 25 hadi 29 Mei, 2026 Mjini Maputo Msumbiji.
Alisema ukame una madhara makubwa katika kilimo, mifugo, rasilimali za maji, usalama wa chakula, maisha ya wananchi, maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.
“Kwa sasa Tanzania inaendelea kuandaa Mpango wa Kitaifa wa Hatua za Mapema dhidi ya ukame kwa msaada wa WFP, kwa kutambua kuwa bado ni moja ya majanga makubwa yanayoathiri nchi yetu,” alisema Dkt. Yonazi.
Aliongeza kuwa mpango huo utawezesha kuwepo kwa mifumo imara ya tahadhari na utekelezaji wa hatua za mapema kabla ya majanga hayajatokea.
Kuhusu ziara hiyo, Dkt. Yonazi alisema Tanzania imechagua kujifunza kutoka Msumbiji kutokana na mafanikio yake katika kuanzisha na kutekeleza mifumo ya hatua za mapema dhidi ya majanga, hususan ukame, mafuriko na vimbunga.
Alisema kupitia ushirikiano huo, Tanzania itanufaika kwa kubadilishana uzoefu na mbinu bora, kujifunza mifumo ya uratibu wa taasisi, vigezo vya kuanzisha hatua za mapema pamoja na namna ya kugharamia hatua hizo.
Aidha, alieleza kuwa uzoefu huo utasaidia kuunganisha hatua za mapema ndani ya mifumo ya hifadhi ya jamii ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na majanga.
“Ziara hii ni muhimu kwa Tanzania katika kujifunza kwa vitendo na kupata mafunzo kutokana na mafanikio ya Msumbiji katika utekelezaji wa hatua za mapema kabla ya maafa,” alisema.
.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)




.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...