Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 7 Mei, 2026 limefanya kikao na wadau wa ujenzi wa meli jijini Mwanza kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa meli na vyombo vingine vya majini nchini ili kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza wakati alipokutana na ujumbe huo, uliongozwa na Wakili Leticia Mutaki, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya Usafiri Majini, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Saidi Mtanda, aliipongeza TASAC kwa kuitisha kikao hicho akisema kuwa kimekuja wakati muafaka kutokana na umuhimu wa sekta ya usafiri majini katika maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Mtanda alisema Mkoa wa Mwanza upo tayari kushirikiana na TASAC katika kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa meli kwa kuwa Mwanza ni lango kuu la usafiri majini katika Ukanda wa Ziwa Victoria na kuwa na meli bora kutasaidia kuimarisha usalama wa usafiri majini.

Aliongeza kuwa zaidi ya asilimia 53 ya eneo la Mkoa wa Mwanza ni maji, hali inayodhihirisha umuhimu wa sekta hiyo kwa uchumi wa mkoa.

Kwa upande wake, Wakili Mutaki akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuhimiza maendeleo ya uchumi wa buluu pamoja na viwanda vya ndani kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Wakili Mutaki aliongeza kuwa TASAC itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa meli na vyombo vya majini nchini ili kupunguza utegemezi wa kuagiza vyombo hivyo kutoka nje ya nchi, hatua ambayo pia itasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Wadau waliohudhuria kikao hicho ikiwemo kampuni za Songoro Marine, Ankola Shipyard Co. Ltd, na Mkombozi Marine waliishukuru TASAC kwa kuandaa kikao hicho na kueleza kuwa kimewapa fursa ya kutambua maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika ujenzi wa meli  pamoja na umuhimu wa kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...