Na Oscar Assenga, Tanga

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imesema kuanzishwa kwa tozo mpya ya maendeleo ya miundombinu ya bandari kutasaidia kuongeza uwezo wa bandari nchini kuhudumia shehena, kupunguza gharama kwa wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza jijini Tanga juzi katika mkutano wa wadau wa watumiaji wa Bandari ya Tanga kuhusu ada ya maendeleo ya miundombinu ya bandari, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, alisema tozo hiyo inayojulikana kama Port Infrastructure Development Levy (PID) ilitarajiwa kuanza kutumika Machi mwaka huu, lakini imeahirishwa hadi Julai Mosi kufuatia maoni ya wadau mbalimbali.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wanachama wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS), ambao waliunga mkono tozo hiyo wakisema italeta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma bandarini nchini.

Mbega alisema lengo la tozo hiyo ni kuboresha miundombinu ya bandari ambayo imeanza kuelemewa kutokana na ongezeko kubwa la shehena katika bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara.

“Bandari ya Tanga kwa sasa inahudumia takribani tani milioni mbili za shehena kwa mwaka, wakati uwezo wa miundombinu iliyopo unatarajiwa kufikia tani milioni tatu ifikapo mwaka 2030. Hata hivyo, kutokana na kasi ya ukuaji wa shehena, kiwango hicho kinaweza kufikiwa mapema mwaka 2027 au 2028,” alisema Mbega.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya usafirishaji imeona umuhimu wa kuwekeza zaidi katika miundombinu ili bandari ziweze kuhimili ongezeko la mizigo.

Mbega alisema fedha zitakazokusanywa kupitia tozo hiyo zitatumika kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali, ikiwemo kuongeza gati jipya katika Bandari ya Tanga.

“Kwa sasa tuna magati mawili, lakini tuna mpango wa kuongeza gati la tatu lenye urefu wa mita 900. Pia eneo la Mwambani lina nafasi kubwa ya kujengwa bandari mpya yenye zaidi ya magati 10 katika eneo la ekari 174,” alisema.

Aliongeza kuwa maboresho hayo yataongeza uwezo wa nchi kuhudumia shehena nyingi zaidi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa mujibu wa Mbega, tozo hiyo pia itasaidia kupunguza gharama wanazopata wafanyabiashara kutokana na ucheleweshaji wa huduma bandarini.

Alisema baadhi ya meli hulazimika kusubiri nje ya bandari kwa muda wa wiki tatu hadi mwezi mmoja kabla ya kuhudumiwa, hali inayosababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara.

“Meli inapokaa nje ya bandari hulipiwa hadi dola za Marekani 20,000 kwa siku. Ukihesabu kwa mwezi mzima ni gharama kubwa sana kwa wafanyabiashara. Tozo hii itasaidia kuongeza ufanisi na kupunguza mzigo huo,” alisema.

Aidha, Mbega alisema maboresho yaliyofanywa kwenye reli ya Tanga kwa gharama ya Sh bilioni 429.1 yameongeza usafirishaji wa mizigo kwenda Rwanda na Burundi.

Alisema reli hiyo ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haitumiki sasa imefunguliwa na kuanza kupokea shehena nyingi kutoka bandarini kwenda Isaka kabla ya kusafirishwa kwenda nchi hizo jirani.

Hata hivyo, alisema ongezeko la mahitaji ya usafirishaji kwa njia ya reli limezidi uwezo wa mabehewa yaliyopo.


“Wateja wanaopendelea kutumia reli wameongezeka zaidi kuliko uwezo wa mabehewa yaliyopo. Huu ni wakati sahihi kwa sekta ya reli kuongeza mabehewa ili kukidhi mahitaji ya soko,” alisema.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TACAS, Ephraim Mwankusye, alisema pendekezo la ada ya asilimia 4.5 ya maendeleo ya miundombinu ya bandari lina lengo la kusaidia maboresho makubwa ya bandari nchini ili kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji wa mizigo.

Alisema fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuendeleza Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara pamoja na Bandari ya Bagamoyo na ujenzi wa miundombinu ya mafuta katika bandari mbalimbali nchini.

Mwankusye alisema lengo kubwa ni kuhakikisha bandari za Tanzania zinakuwa za kisasa, zenye uwezo mkubwa wa kuhudumia mizigo mingi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Kwa mujibu wa pendekezo hilo, asilimia 4.5 ya tozo ya PID itaelekezwa katika miradi ya kuboresha bandari, magati, reli, matenki ya mafuta pamoja na barabara zinazosaidia usafirishaji wa mizigo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...