Vodacom M-Pesa Tanzania imetangaza ushirikiano mpya na PayPal ambao utawezesha wateja nchini Tanzania kufanya miamala kwa urahisi kati ya akaunti zao za PayPal na pochi za M-Pesa kupitia M-Pesa Super App. Kama sehemu ya suluhisho pana la malipo ya kimataifa la M-Pesa, hatua hii inaashiria maendeleo muhimu katika kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali za kimataifa.

Kupitia mfumo huu mpya, wateja wa M-Pesa watakaokidhi vigezo wataweza kuweka fedha moja kwa moja kwenye akaunti zao za PayPal na pia kutoa fedha kutoka PayPal kwenda kwenye akaunti zao za M-Pesa kwa njia salama na rahisi zaidiHuduma hii inaenda kurahisisha miamala ya kimataifa kwa wafanyakazi wa kujitegemea (freelancers), watengeneza maudhui, wajisiriamali wanaoshiriki uchumi wa kazi za muda (gig economy), pamoja na Watanzania wengine waliounganishwa kidijitali.

Ushirikiano huu unakuja wakati mahitaji ya huduma rahisi za malipo ya kuvuka mipaka yanaendelea kuongezeka miongoni mwa Watanzania wanaoshiriki katika biashara za kimataifa, kazi za kujitegemea na huduma za kidijitali. Kupitia huduma hii ya kuwezesha utoaji wa fedha kutoka PayPal kwenda M-Pesa, Watanzania sasa wataweza kupata na kutumia mapato yao ya PayPal kwa urahisi zaidi.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa, Tulisindo Mlupilo, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira endelevu ya M-Pesa ya kuwaunganisha wateja na fursa zaidi kupitia ubunifu na huduma jumuishi za kifedha.

“Uunganisho wa kidijitali unaendelea kufungua fursa nyingi zaidi kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa kimataifa kupitia biashara za mtandaoni, kazi za kujitegemea, utengenezaji wa maudhui na biashara za kuvuka mipaka. Kupitia ushirikiano huu na PayPal, tunawarahisishia zaidi wateja wetu kutuma, kupokea, na kutoa fedha kati ya mifumo hii kwa urahisi na uhakika zaidi,” alisema Mlupilo.

Otto Williams, Makamu wa Rais Mwandamizi, Mkuu wa Kanda na Meneja Mkuu wa Mashariki ya Kati na Afrika wa PayPal, alisema ushirikiano huo unawezesha muingiliano mkubwa zaidi wa mifumo kwa wateja wanaofanya miamala ya kidijitali ya kimataifa

“Duniani kote, tunaendelea kushuhudia ukuaji wa biashara za kidijitali pamoja na ongezeko la ushiriki wa watu katika kazi za mtandaoni. Kwa kuwezesha uhamishaji rahisi wa fedha kati ya PayPal na M-Pesa kupitia kuunganisha akaunti, ushirikiano huu utasaidia kutoa huduma ya malipo ya kuvuka mipaka iliyo rahisi, salama na yenye ufanisi zaidi kwa wateja nchini Tanzania,” alisema Williams.

Wateja wataweza kutumia huduma hiyo moja kwa moja kupitia M-Pesa Super App kwa kuunganisha akaunti zao za PayPal na akaunti zao za M-Pesa kupitia mfumo rahisi wa usajili na uthibitishaji utakaowezesha miamala salama na rahisi kati ya mifumo hiyo miwili.

Ushirikiano huu unaendelea kuimarisha nafasi ya M-Pesa kama kinara wa huduma za kifedha za kidijitali na ubunifu nchini Tanzania, huku ukiunga mkono juhudi pana za kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa kidijitali.

Maelezo zaidi kuhusu namna ya kujiunga na huduma hii, viwango vya miamala, muda wa kuanza kwa huduma pamoja na mwongozo wa matumizi yatatolewa kupitia:tovuti rasmi ya Vodacom Tanzania na njia nyingine rasmi za mawasiliano za M-Pesa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...