• Mapato ya huduma yaongezeka kwa asilimia 21.8 yakichangiwa na ongezeko la wateja na matumizi makubwa ya huduma.

• Faida halisi yavuka shilingi 200 bilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 125.5 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

• Uwekezaji wa juu zaidi kuwahi kufanyika wa shilingi 323.9 bilioni katika gharama za uwekezaji (capex), ikiwa ni ongezeko la asilimia 85.1 ulielekezwa katika upanuzi wa huduma za intaneti yenye kasi na maboresho ya miundombinu ya teknolojia.

• Mwelekeo mzuri katika kuendeleza ujumuishaji wa kifedha:

o Mikopo midogo yenye thamani ya zaidi ya shilingi 3 trilioni ilitolewa.

o Amana za M-Koba ziliongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 na kuvuka Shilingi trilioni moja.

o M-Wekeza ilitoa fursa ya uwekezaji kwa maelfu ya wateja, huku thamani ya uwekezaji ikizidi shilingi 370 bilioni ndani ya kipindi kisichozidi miaka miwili.


Dar es Salaam, Tanzania – 8 Mei 2026: Vodacom Tanzania PLC leo imetangaza ukuaji mkubwa wa faida kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Machi 2026, hatua inayoonesha ubora katika utekelezaji wa mikakati, usimamizi madhubuti wa gharama na uwekezaji endelevu katika mtandao na jukwaa la huduma za fedha kwa simu. Utendaji huo umechangiwa na ukuaji mkubwa wa mapato ya huduma pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa mbalimbali katika makundi yote ya wateja.

Matokeo hayo yanaonyesha dhamira endelevu ya Vodacom katika kuhakikisha ukuaji wenye faida na uundaji wa thamani ya muda mrefu, huku ikiendelea kuwekeza katika kuimarisha ubora wa mtandao, kupanua huduma za kidijitali na kusaidia maendeleo jumuishi ya kiuchumi nchini Tanzania.

Ikiwa ni kampuni pekee ya mawasiliano iliyoorodheshwa katika soko la hisa nchini, Vodacom imeonyesha uthabiti wa utendaji wake wa kifedha na uwazi licha ya changamoto za kijiografia za kisiasa duniani na misukosuko ya sekta. Kampuni hiyo imesisitiza nafasi yake kama mshirika wa kuaminika wa kibiashara na mdau mwenye mchango wa uwajibikaji katika maendeleo ya taifa, ikiwa imeendelea kufanya shughuli zake hapa nchini chini ya chapa ya Vodacom kwa miaka 25 mfululizo.

Akizungumza kuhusu matokeo ya awali ya kifedha kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Machi 2026, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire, alisema kampuni imepata faida kutokana na utekelezaji bora wa mikakati na mazingira thabiti ya biashara.

Mapato ya huduma yaliongezeka kwa asilimia 21.8 hadi kufikia shilingi 1.85 trilioni, yakichangiwa na ongezeko la wateja pamoja na matumizi makubwa ya huduma. Kutokana na hali hiyo, faida halisi baada ya kodi iliongezeka kwa asilimia 18.4 hadi kufikia shilingi 107.1 bilioni, huku faida halisi ikifikia shilingi 204.1 bilioni baada ya kuondoa gharama za maboresho ya mtandao wa mawasiliano ya redio. Hii inaonesha kasi endelevu katika vyanzo vikuu vya mapato vya Vodacom pamoja na udhibiti madhubuti wa gharama.

“Utendaji wetu mzuri unatokana na maamuzi ya makusudi ya uwekezaji pamoja na kuendelea kuzingatia upanuzi wa huduma zinazotoa thamani kwa wateja wetu na wanahisa. Idadi ya wateja wetu iliongezeka kwa asilimia 22.3 na tumeendelea kushikilia nafasi yetu kama kinara wa soko,” alisema Bw. Besiimire.

Mtendaji Mkuu aliongeza kuwa, “mapato ya M-Pesa yaliongezeka kwa asilimia 24.5 yakichangiwa na kuongezeka kwa matumizi ya huduma zetu kama mikopo, akiba na malipo kwa wafanyabiashara, huku mapato ya huduma za intaneti yakiongezeka kwa asilimia 29.5 kutokana na ongezeko la watumiaji wa simu janja, likiungwa mkono na uwekezaji uliofanyika.”

Ikiwa inaongozwa na dhamira yake ya kuwaunganisha Watanzania kwa mustakabali bora zaidi, Vodacom imeendelea kuwekeza katika miradi yenye matokeo chanya kwa jamii, ikiwemo kambi za uchunguzi wa afya bila malipo, maboresho ya TEHAMA mashuleni, programu za upandaji miti pamoja na msafara wa baiskeli (Twende Butiama), hatua zilizosaidia kuimarisha ushiriki wa jamii na athari chanya za kijamii.

Kwa kuangazia mbele, Vodacom Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya mtandao, upanuzi wa huduma za kifedha na biashara pamoja na kuboresha uzoefu wa wateja. Aidha, kampuni inalenga kuendelea kuoanisha mkakati wake na mipango ya maendeleo ya taifa pamoja na ajenda ya mageuzi ya kidijitali, kwa kutumia uongozi wake wa kiteknolojia na nafasi yake imara sokoni.

Bw. Besiimire alisisitiza dhamira ya Vodacom katika kuhakikisha ukuaji endelevu, uendeshaji unaozingatia maadili, utunzaji wa mazingira na kuendelea kujenga imani, huku akieleza kuwa uwekezaji unaoendelea katika miundombinu utatoa thamani ya muda mrefu kwa wateja, wanahisa na taifa kwa ujumla.

“Tunapoangazia siku zijazo, tunaendelea kuwa na dhamira ya kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine wanaosaidia ajenda ya maendeleo ya Tanzania na kujenga jamii jumuishi ya kidijitali,” alihitimisha Bw. Besiimire.

Matokeo kamili: www.vodacom.co.tz/financials



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...