Na Mwandishi Wetu
MWENYEKI wa Chama cha mawakili wa Serikali, Addo November amesema mbio za Wakili Marathon zitakazofanyika Mei 31 mwaka huu mjini Dodoma zinalenga kuhamasisha utoaji wa msaada wa kisheria pamoja na kuwajengea Watanzania utamaduni wa kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 17,2026 Jijini Dar es salaam, November amesema mbio hizo zitawakutanisha viongozi wa serikali, mawakili, wanamichezo na wananchi wa kawaida katika kuunga mkono kampeni ya msaada wa kisheria inayotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Samia Legal Aid Campaign.

Amesema hadi sasa mamilioni ya Watanzania tayari wamefikiwa na huduma za msaada wa kisheria bure, huku changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wengi zikiwa ni migogoro ya ardhi, ndoa pamoja na unyanyasaji wa aina mbalimbali, jambo lililoifanya jamii kuendelea kuhitaji msaada huo muhimu.

November ameeleza kuwa marathon hiyo itakuwa na mbio za kilomita 21 pamoja na mbio za umbali mfupi kwa washiriki wa rika tofauti, huku watoto nao wakitengewa nafasi maalumu ya kushiriki ili kukuza vipaji vya michezo tangu wakiwa wadogo.

Aidha amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika ikiwemo uwepo wa huduma za afya kutoka Shirika la Red Cross, vituo vya maji na matunda kwa washiriki pamoja na utoaji wa medali na zawadi kwa washindi wa mashindano hayo.

Aidha November amesema washiriki watatakiwa kulipia Sh40,000 kwa ajili ya usajili ambapo watapatiwa vifaa mbalimbali vya marathon hiyo, huku akibainisha kuwa lengo la awali ni kupata washiriki zaidi ya 5,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa mbio hizo zitapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali pamoja na uwepo wa viongozi wa kitaifa akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari huku majina mengine ya wageni maalumu yakiendelea kutangazwa kadri siku zinavyosogea.

Naye mwanariadha mstaafu, Juma Ikangaa amesema marathon hiyo itasaidia kuibua vipaji vipya vya riadha nchini na kuongeza hamasa ya Watanzania kushiriki michezo kwa manufaa ya afya na maendeleo ya taifa.

Amesema ushiriki wa wanasheria katika mbio hizo unaonyesha namna taaluma hiyo ilivyo tayari kushirikiana na jamii katika shughuli za maendeleo, huku akiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo la kihistoria litakalofanyika katika Viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...