Walimu nchini wametakiwa kuchukua jukumu kubwa katika kujenga kizazi chenye uelewa wa teknolojia na matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali ili kuiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na uchumi wa kidijitali.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati, Mhandisi Asajile John, wakati wa mkutano na wadau wa elimu uliofanyika Mei 6, 2026 jijini Dodoma, amesema walimu wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa sahihi ya teknolojia tangu ngazi za awali.

Amesisitiza kuwa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye uwezo wa kushindana katika dunia ya kidijitali, aidha amezihimiza shule kuanzisha vilabu vya kidijitali vitakavyowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo, kujadiliana na kukuza ubunifu wao.

“Nadhani kama zilivyo Klabu za rushwa, hisabati n.k, nadhani ni wakati sasa wa shule kuanzisha vilabu vya kidijitali ili kuwajengea wanafunzi uelewa mpana wa teknolojia na kuwasaidia kuwa kuwajenga kuanzia ngazi ya awali”.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mhandisi Asajile alibainisha kuwa inalenga kufikia angalau asilimia 70 ya Watanzania kuwa na uelewa wa matumizi ya teknolojia ya kidijitali, pamoja na kuhakikisha huduma nyingi zinaunganishwa katika mifumo ya kidijitali ili kuongeza tija.

Katika mkutano huo, pia aliwakumbusha wananchi kuwa makini na matumizi ya simu zao, akieleza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu kumekuwepo na takribani majaribio ya uhalifu 9,800 kupitia ujumbe wa “tuma pesa kwa namba hii”.

Ameonya kuwa baadhi ya wahalifu hutumia laini zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine, hivyo wananchi wanapaswa kulinda laini zao kwani usajili wake ni mkataba wa kisheria unaohusisha namba ya NIDA na alama za vidole.

“Laini yako ni jukumu lako, Hakikisha haitumiki vibaya kwani unaweza kujikuta unaingia kwenye matatizo ya kisheria bila sababu,”.

Amehitimisha kwa kusema kuwa matumizi sahihi ya teknolojia ya mawasiliano yanaweza kurahisisha maisha, kuokoa muda na kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.




 

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...