📍TRA yawawekea mkakati rafiki wa Kodi

Na MASHAKA MHANDO, Tanga


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga, imebainisha kuwa wanawake nchini wanamiliki asilimia 54 ya biashara ndogo, za kati na ndogo (MSMEs), hali inayolazimu kuwepo kwa mifumo rafiki ya kodi itakayochochea ukuaji wa sekta hiyo bila hofu ya vikwazo.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 14, 2026, na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, John Castro wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi lililofanyika katika ukumbi wa Regal Naivera Hotel jijini hapa.

John alisema takwimu za hivi karibuni zinaonyesha mchango mkubwa wa wanawake katika uchumi, ambapo ushiriki wao katika nguvu kazi unakadiriwa kufikia takribani asilimia 80 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jambo linalowafanya kuwa mhimili mkuu wa mapato ya ndani.

Jukwaa la Wanawake na Kodi

Meneja huyo alifafanua kuwa kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni hatua ya kihistoria yenye lengo la kuwapa wanawake elimu sahihi, kusikiliza changamoto zao, na kujenga uaminifu utakaohamasisha ulipaji kodi kwa hiari badala ya kutumia nguvu.

"Tunatambua kuwa mwanamke akisimama kiuchumi, familia inaimarika na Taifa linapiga hatua. TRA imejikita kuboresha huduma kwa weledi na uwazi ili mwanamke ajisikie salama na anaheshimiwa anaposhiriki katika mfumo wa kodi," alisema John.




Kodi na Miradi ya Kimkakati

John alisisitiza kuwa kodi ndiyo injini inayogharamia miradi ya kimkakati nchini ikiwemo afya, elimu, barabara na maji, hivyo mwanamke anayelipa kodi anakuwa mshirika wa moja kwa moja wa Serikali katika ujenzi wa Taifa.

Aidha, aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Tanga chini ya Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian na wadau wa maendeleo kama GIZ, kwa kuweka mazingira yanayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kupata elimu ya kodi.

Wito kwa Wadau na Taasisi za Fedha

Katika kongamano hilo, TRA imetoa wito kwa taasisi za kifedha kushirikiana na Mamlaka hiyo wakati wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wanawake, ili waweze kupewa elimu ya kodi sambamba na mitaji, jambo litakalosaidia biashara zao kuimarika na kuwa endelevu.

Pia, aliwataka wanawake wote mkoani Tanga kujisajili katika mfumo wa kodi na kutumia madawati ya uwezeshaji biashara yaliyopo katika kila ofisi ya TRA ili kupata ushauri wa kitalamu wa kibiashara.

Mmoja ya washiriki wa kongamano Hilo, kutoka kampuni ya Maluu Smart Production, Hadija Mohamed, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga kwa kuanzisha jukwaa hilo, akisema limekuwa mkombozi katika kufungua macho ya wanawake wajasiriamali kuhusu mnyororo wa kodi na fursa za kibiashara. Hadija amebainisha kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuendesha biashara zao kwa weledi na kuondoa hofu ya awali waliyokuwa nayo dhidi ya kodi, jambo litakalopelekea uzalishaji wenye tija na kufuata sheria za nchi kitalamu.

Aidha, Hadija amesisitiza kuwa kupitia mafunzo hayo, Maluu Smart Production imejipanga kuwa balozi wa utii wa kodi kwa hiari, huku akiiomba TRA kuendelea kutoa huduma za ushauri wa karibu kwa viwanda vidogo ili viweze kukua na kufikia soko la kimataifa. Amesema kuwa kutambuliwa kwa mchango wa mwanamke katika uchumi kupitia kongamano hilo ni ishara tosha ya ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza mapato ya ndani na maendeleo ya kijamii.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...