▪️Asema migogoro ya ardhi inahitaji suluhisho la kudumu la kitaasisi

▪️Asisitiza mifumo ya utatuzi wa migogoro iimarishwe

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka, kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

“Utaratibu mzuri wa utawala bora ni ule wa kitaasisi, unaowezesha wananchi kupata haki zao kupitia mifumo imara,” amesema Dkt. Nchemba.

Amesema hayo leo Jumatano, Mei 20, 2026 wakati akisikiliza na kushughulikia kero za wananchi wa maeneo ya Mahomanyika, Ndachi, Mbuyuni na Nkuhungu Broad Acres katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Kikao hicho kilihusisha viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jiji la Dodoma pamoja na wataalamu wa ardhi kutoka ngazi mbalimbali za Serikali.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alipokea taarifa za kina kuhusu hali ya migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kushughulikia migogoro hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ipo haja ya kufanya mapitio ya kina ya mfumo wa mabaraza ya ardhi kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika upatikanaji wa huduma za mahakama nchini.

Amesema wakati mfumo huo unaanzishwa, lengo lilikuwa kusogeza huduma karibu na wananchi, lakini kwa sasa mahakama zimeenea katika maeneo mengi zaidi hali inayotoa fursa ya kutathmini upya ufanisi wa mfumo huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera amesema tayari Serikali imeandaa hati ya mwongozo wa namna ya kushughulikia kesi za ardhi kupitia mahakama na kwamba hatua zilizobaki ni kukamilisha taratibu za uwasilishaji kwa mamlaka husika.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesema ongezeko la thamani ya ardhi Jijini Dodoma baada ya Serikali kuhamia Makao Makuu limechangia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi, uvamizi wa maeneo pamoja na biashara holela ya viwanja.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya amesema Serikali itaendelea kushughulikia migogoro hiyo kwa kuzingatia sheria, haki na maslahi ya wananchi huku ikiendelea kulinda maeneo ya umma dhidi ya uvamizi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...