📌 Utawezesha Mkoa wote Kagera kuunganishwa na Gridi ya Taifa
📌 Zaidi ya Bilioni 270 kutumika kutekeleza mradi
📌 Mradi kukamilika ndani ya miezi 24
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi leo Mei 9, 2026 ameweka jiwe la msingi la mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa KV 220 Benaco–Kyaka pamoja na Kituo cha Kupoza Umeme cha Benaco wilayani Ngara, mkoani Kagera.
''Tunatarajia ndani ya miezi 24 Mkoa wa Kagera uwe umeunganishwa katika Gridi ya Taifa na changamoto za umeme ziwe historia,” alisema Mhe. Ndejembi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Bw. Mathias Kahabi, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Nishati kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo ya umeme wilayani humo.
Amesema katika Jimbo la Ngara vijiji vyote 75 tayari vimefikiwa na huduma ya umeme, huku vitongoji 219 kati ya vitongoji 389 vikiwa tayari vimeunganishiwa umeme.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange amesema mradi huo utaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi Mkoa wa Kagera.
“TANESCO imejipanga kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa,” alisema Bw. Twange.
Naye Mjumbe wa Bodi ya TANESCO, Bi. Zuhura Bundala amesema mradi huo utafungua fursa za maendeleo, ajira kwa vijana na kuongeza uzalishaji mali kwa wananchi wa Kagera.
“Mradi huu utafungua fursa nyingi za maendeleo kwa wananchi wa Kagera,” alimalizia Bi. Bundala.
Katika hatua nyingine Waziri Ndejembi ameuagiza uongozi wa TANESCO kuhakikisha wananchi hawaendelei kusubiri huduma ya umeme kwa muda mrefu kwa kutafuta transfoma kubwa zitakazosaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea.
Sambamba na hilo, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati bila ucheleweshaji, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa ajira kwa wananchi wa maeneo husika pamoja na kulipa fidia stahiki kwa waliopisha utekelezaji wa mradi.
“Niwatake wakandarasi kukamilisha mradi huu kwa wakati bila ucheleweshaji wowote. Vilevile, hakikisheni wananchi wanapata ajira kupitia utekelezaji wa mradi huu pamoja na kulipwa fidia zao kwa wakati,” amesema Ndejembi.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...