*China yafungua mlango wa ushuru sifuri kwa bidhaa za Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imesema itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi ili wanufaike kikamilifu na fursa za masoko ya kimataifa na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo Kapinga, wakati wa mkutano wa wadau kuhusu matumizi ya fursa ya kuuza bidhaa nchini China bila ushuru, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Kapinga amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa unalenga kuwaunganisha wasafirishaji wa bidhaa kwenda China na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinafikia masoko ya kimataifa kwa ushindani mkubwa.

Amesema serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwawezesha wafanyabiashara katika kila hatua ili kutimiza azma ya kukuza diplomasia ya uchumi na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.

“Tunachojadili hapa kisiwekwe kabatini. Wafanyabiashara wanahitaji kutatuliwa changamoto zao ili waweze kutumia fursa zilizopo,” amesema Kapinga.

Aidha, amesema mfanyabiashara hapaswi kuambiwa hana vigezo vya kushiriki soko la kimataifa, bali juhudi zinapaswa kuelekezwa katika kumwezesha kufikia viwango vinavyotakiwa kwa biashara hizo.

Kapinga ameihimiza sekta binafsi kujipanga kutumia soko la China, akieleza kuwa mazingira yaliyowekwa ya kuingiza bidhaa bila ushuru yanafungua fursa kubwa kwa wazalishaji na wasafirishaji wa Tanzania.

Amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwekeza katika ubora wa bidhaa, kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha usindikaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Kwa mujibu wa Kapinga, kupitia mifumo mbalimbali ya biashara ya upendeleo, bidhaa nyingi zinazozalishwa Tanzania zinaweza kuingia katika masoko makubwa duniani bila ushuru au kwa masharti nafuu ya ushuru, jambo linaloongeza ushindani wake katika soko la dunia.

Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara kuzingatia kanuni za asili ya bidhaa kwa kuhakikisha bidhaa zinazouzwa nje zimezalishwa nchini au zimeongezewa thamani kwa kiwango kinachokubalika kimataifa.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania amesema hamasa iliyooneshwa na washiriki wa mkutano huo inaashiria nia kubwa ya wafanyabiashara kutumia fursa hiyo, japokuwa bado kuna changamoto ya uelewa wa sera na namna bora ya kuitumia kwa vitendo.

Amesema China itaendelea kushikilia sera ya urafiki, uaminifu na ushirikiano wa dhati kwa kutumia mpango wa ushuru wa sifuri kama nyenzo ya kuimarisha biashara na maendeleo ya pamoja kati ya China, Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Aidha, amesema Serikali ya China imeanza utekelezaji wa sera ya ushuru wa sifuri kwa nchi 20 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China ambazo hazipo katika kundi la nchi maskini zaidi duniani, huku mpango huo ukitarajiwa kudumu kwa miaka miwili.

Naye Mshauri wa Rais wa Masuala ya Kilimo, Geoffrey Kirenga, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na soko hilo kutokana na uzalishaji wa bidhaa bora zikiwemo korosho, kahawa na viungo.

Kirenga amesema tayari uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani unaendelea, sambamba na ununuzi wa mashine za kisasa kutoka China, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Kapinga ameagiza TanTrade kuweka mikakati endelevu ya kuwawezesha wafanyabiashara ili Tanzania iwe kitovu cha biashara ya kimataifa na uzalishaji wa viwanda wenye ushindani katika ukanda wa Afrika Mashariki.



Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...