Na. Jawadu Kinyobwa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Wahitimu wa Taasisi ya Uongozi kuwa waadilifu, wenye nidhamu na uthubutu ili kuleta maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.
Mhe. Ridhiwani amebainisha hayo Mei 15, 2026 katika Sherehe ya Tisa ya Mahafali ya Taasisi ya Uongozi yaliyofanyika Mlimani City, Jijini Dar es salaam.



Aidha, amesema katika ulimwengu wa sasa uadilifu ndio sifa kuu ya kiongozi bora na mwenye kuaminika, hivyo watumie maarifa na ujuzi walioupata chuoni kuwa viongozi wanaozingatia haki, uwajibikaji na weledi katika kila jambo.



“Nawakumbusha umuhimu wa kuwa Viongozi Wenye Uzalendo. Tukumbuke msemo wa wahenga: Adhabu ya msaliti ni malipo ya usaliti wake. Usaliti mkubwa katika uongozi wa umma ni sawa na ubadhirifu wa mali za Umma” amesema.



Akizungumza kuhusu umuhimu wa uadilifu katika uongozi, amewasihi wahitimu hao kuwa viongozi wenye maadili mema, wanaolinda mali za umma na kuweka mbele maslahi ya wananchi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.



Amesema Taifa linahitaji viongozi waaminifu, wenye uwajibikaji na wanaotumia nafasi zao kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya Watanzania wote.


Sambamba na hayo, Mhe. Ridhiwani amesisitiza kuwa, uongozi bora na wa kuzingatia misingi ya haki na uwazi utasaidia kuendelea kuitangaza vyema Tanzania pamoja na Taasisi ya Uongozi ndani na nje ya nchi.

Awali akizungumza Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Bw. Kadari Singo, amesema Taasisi hiyo imetimiza miaka kumi na tano tangu ilipoanzishwa rasmi Julai 2010 kwa Hati ya Rais kama Kituo cha Utaalamu wa Hali ya Juu (Centre of Excellence) cha kujenga na kuimarisha viongozi barani Afrika ili kuleta maendeleo endelevu.



Amebainisha kuwa, Taasisi hiyo imeendelea kufanya kazi kubwa na nzuri katika utoaji wa programu za mafunzo ya uongozi, uandaaji wa mijadala ya kisera, upanuzi wa dimbwi la maarifa kupitia tafiti na machapisho mbalimbali.



Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika fikra, uwezo wa uongozi na namna ya kufanya maamuzi yenye tija kwa taasisi na jamii.



Amesema mahafali hayo hayakuwa tu sherehe ya kukamilisha mafunzo, bali yalikuwa ishara ya mabadiliko na ukuaji wa kiuongozi walioupata washiriki ndani ya kipindi cha miezi sita ya programu hiyo.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...