Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Wizara ya Uchukuzi imewasilisha ombi la kuidhinishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi 2,872,738,082,000 kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya kuimarisha na kuendeleza sekta ya uchukuzi nchini.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, kati ya fedha hizo, Shilingi 126,041,236,000 zimetengwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, huku Shilingi 2,746,696,846,000 zikielekezwa katika Miradi ya Maendeleo, ikilenga kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, reli, barabara na huduma nyingine za uchukuzi.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa bajeti hiyo imelenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya sekta ya uchukuzi nchini, sambamba na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri.
Ameeleza kuwa pamoja na hotuba hiyo, wizara imeambatisha majedwali mbalimbali yenye takwimu na taarifa za kina ili kutoa uelewa mpana zaidi kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kuhusu hali ya utekelezaji wa sekta hiyo.
Aidha, amesema majedwali hayo ni sehemu ya hotuba rasmi ya bajeti na yanapatikana pia kupitia tovuti ya Wizara ya Uchukuzi kwa ajili ya rejea ya umma kupitia www.uchukuzi.go.tz.
Wizara hiyo inaendelea kuweka mkazo katika kuboresha miundombinu ya uchukuzi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...