Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Serikali imewataka vijana wa Kitanzania kujiepusha na ushawishi wa kujiingiza katika migogoro ya kivita ya kimataifa kwa lengo la kutafuta kipato, ikionya kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria na inaweza kuhatarisha maisha yao.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ngwaru Maghembe wakati akijibu swali la Mbunge Jesca John Magufuli aliyehoji Serikali ina mkakati gani wa kujenga uelewa kwa vijana kuhusu athari za kushiriki katika migogoro ya kimataifa, ikiwemo vita kati ya Ukraine na Urusi.

Dkt. Maghembe amesema katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo na mwenendo wa baadhi ya vijana, hususan kutoka Bara la Afrika, kuhamasishwa kujiunga na majeshi ya nchi zinazokabiliwa na migogoro ya kivita kwa ahadi ya ajira na kipato bora kutokana na changamoto za ukosefu wa ajira katika nchi zao.

Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutoa elimu ya uraia na kuongeza uelewa kwa vijana kuhusu madhara ya kujiingiza katika vita vya nje, ikisisitiza kuwa kushiriki katika migogoro hiyo bila utaratibu rasmi ni kinyume cha sheria za Tanzania pamoja na sheria za kimataifa.

“Vijana wanapaswa kuelewa kuwa migogoro ya kimataifa ina athari kubwa kiusalama, kijamii na kiuchumi, na kwa baadhi inaweza kusababisha vifo, majeraha makubwa au ulemavu wa kudumu,” amesema Dkt. Maghembe.

Ameeleza kuwa juhudi hizo zinaongozwa na miongozo mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la 2024 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambazo zinahimiza usalama, ustawi wa vijana na ushiriki wao katika shughuli halali za maendeleo.

Wakati huo huo, Serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa ajira salama kwa vijana nje ya nchi kupitia mikataba ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa inayolenga kuhakikisha Watanzania wanapata fursa za kazi katika mazingira yanayolindwa kisheria.

Dkt. Maghembe amesema katika mwaka huu wa fedha, Serikali imefanikisha upatikanaji wa nafasi 1,500 za ajira kwa madereva nchini Qatar pamoja na nafasi nyingine 300 za wauguzi nchini Saudi Arabia.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kiuchumi, ikiwemo kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya vijana sambamba na programu maalum za kisekta zinazolenga kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na ajira rasmi.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha vijana kutumia fursa halali za kiuchumi zilizopo ndani na nje ya nchi badala ya kujiingiza katika shughuli zinazoweza kuhatarisha usalama na mustakabali wao.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...