Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni Dodoma.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi 137,812,633,000 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kukuza uchumi wa viwanda na kuimarisha mazingira ya biashara nchini.
Waziri Kapinga ameyasema hayo leo bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akieleza kuwa fedha hizo zitasaidia kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya viwanda, biashara, uwekezaji pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.
Amesema kati ya fedha zinazoombwa, shilingi 104,122,530,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya Wizara, huku shilingi 33,690,103,000 zikitengwa kwa matumizi ya maendeleo yanayolenga kuimarisha miradi na shughuli mbalimbali za kimkakati ndani ya sekta hiyo.
Akifafanua zaidi kuhusu matumizi ya kawaida, Waziri Kapinga amesema jumla ya shilingi 78,049,345,000 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa Wizara na taasisi zake, huku shilingi 26,073,185,000 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo ikiwemo uendeshaji wa shughuli za kila siku, usimamizi wa programu mbalimbali pamoja na utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika maeneo tofauti nchini.
Kwa upande wa bajeti ya maendeleo, Waziri huyo amesema fedha zote za maendeleo zinazotarajiwa kutumika katika mwaka huo wa fedha ni fedha za ndani, jambo alilosema linaonesha dhamira ya Serikali ya kujitegemea katika kugharamia miradi ya maendeleo na kuendelea kuimarisha uchumi wa taifa kupitia sekta ya viwanda na biashara.
Aidha, Waziri Kapinga amesema Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza uzalishaji wa viwandani, kuvutia uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi, hususan vijana.
Katika hotuba yake, Waziri huyo pia alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kufanikisha agenda ya maendeleo ya viwanda nchini, akibainisha kuwa mazingira bora ya biashara yanaendelea kuboreshwa ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hilo, amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya biashara, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuhakikisha viwanda vya ndani vinapata mazingira rafiki ya uzalishaji na biashara.
Waziri Kapinga ameongeza kuwa wananchi na wadau mbalimbali wanaweza kupata hotuba hiyo kwa undani zaidi kupitia tovuti rasmi ya Wizara ya Viwanda na Biashara.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...