Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma

Mbunge wa Kigoma Mjini Clayton Revocatus Chipando (Baba levo) ameishauri Serikali na Bunge kufanya mapitio ya mfumo wa utozaji tozo katika sekta ya bodaboda, akisisitiza kuwa kundi hilo kubwa la vijana haliwezi kubebeshwa mzigo mpya wa kodi kutokana na hali yao ya kiuchumi.

Akichangia mjadala wa bajeti kuu ya Serikali, Chipando amesema bodaboda ni moja ya sekta zinazowezesha maisha ya mamilioni ya Watanzania, na kuongeza gharama mpya kutawaumiza zaidi wananchi walioko katika kipato cha chini.

Ameeleza kuwa takribani asilimia 75 ya waendesha bodaboda nchini ni vijana waliomaliza elimu ya msingi, hususan darasa la saba, ambao hawakuweza kuingia katika ajira rasmi, hivyo kujikuta wakijiajiri kwenye sekta isiyo rasmi ili kujikimu kimaisha.

Amesema badala ya kuongeza tozo katika sekta hiyo, Serikali inapaswa kutafuta vyanzo vingine vya mapato visivyoathiri moja kwa moja wananchi wenye kipato kidogo, huku akilinganisha hali hiyo na ongezeko la gharama katika bidhaa nyingine ambazo hazina athari kubwa kwa kundi hilo.

Katika hoja nyingine, mbunge huyo ameitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye teknolojia ya kisasa katika sekta ya ulinzi, ikiwemo matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone) na vifaa vya kisasa vya kijeshi, ili kuendana na mabadiliko ya vita vya kisasa duniani, akitolea mfano wa migogoro kama ya Ukraine.

Aidha, katika sekta ya michezo na sanaa, Chipando amependekeza taasisi za kifedha kuwapa wasanii muda wa kutosha wa kurejesha mikopo wanayopewa kupitia programu za Serikali. Ameomba muda wa angalau miezi mitatu hadi sita ili kuwapa nafasi ya kurejesha mikopo baada ya kazi zao kuanza kuleta kipato.

Pia amesisitiza kuwa mikopo hiyo, ambayo hutolewa kupitia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, inapaswa kuwa na masharti rafiki yanayolenga kuwawezesha walengwa kunufaika badala ya kubanwa na ratiba ngumu za marejesho.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...