Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, amesema lengo la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni kuwawezesha wananchi wanaoishi katika mazingira magumu na kaya maskini kujikwamua kiuchumi, kufikia ndoto zao na kuboresha maisha yao kwa kujitegemea.
Regina ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akitembelea banda la TASAF katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Amesema TASAF imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na mfuko huo, hatua ambayo imeongeza uelewa kwa kaya maskini na kuwasaidia kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
"Nawapongeza TASAF kwa kazi nzuri mnayoifanya. Msichoke kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu ya kuwainua wananchi kiuchumi na kuifanya Tanzania kuwa imara kwa kuwawezesha watu kujitegemea badala ya kutegemea misaada," amesema Regina.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameipongeza TASAF kwa kuendelea kutoa msaada wa elimu kwa watoto kutoka katika kaya maskini, jambo ambalo limechangia kuwawezesha kuendelea na masomo yao huku familia zao zikipata nafuu ya changamoto za kiuchumi.
Amesema uwekezaji katika elimu kupitia TASAF umekuwa na mchango mkubwa katika kujenga mustakabali bora wa watoto wanaotoka katika mazingira yenye uhitaji mkubwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Gift Msuya, amesema viongozi wa wilaya hukutana na watoto wengi wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma lakini wanakabiliwa na changamoto za kifedha zinazowazuia kufikia malengo yao ya elimu.
Kutokana na hali hiyo, ameshauri TASAF kuangalia uwezekano wa kuwa na mfumo utakaotambua kaya zenye uhitaji kupitia mamlaka za serikali za mitaa, ikiwemo zile zilizopo maeneo ya mijini ambazo mara nyingi hushindwa kuingia kwenye mifumo ya TASAF kupitia utaratibu wa kawaida wa usajili.
"Tuna kaya nyingi zenye uhitaji mkubwa mijini ambazo hazijafikiwa na programu za TASAF. Ni muhimu kuangalia namna ya kuzitambua na kuzifikia ili nazo zipate fursa ya kunufaika na huduma hizi," amesema Msuya.
Aidha, ameomba TASAF kuzingatia zaidi kaya zenye watoto yatima waliofiwa na wazazi wao, ili waweze kupata msaada unaohitajika na kuendelea na masomo pamoja na maisha yao ya kila siku bila vikwazo vikubwa vya kiuchumi.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi mbalimbali za serikali kuonyesha huduma wanazotoa kwa wananchi pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha ustawi wa jamii.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...