Na Belinda Joseph-Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua rasmi Mwongozo wa Uendeshaji wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Toleo la Pili, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na ufanisi wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Juni 25, 2026, Jijini Dodoma, alisema mwongozo huo utasaidia kuongeza uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya viongozi na wanachama wa NaCoNGO, amebainisha kuwa uwepo wa taratibu zilizo wazi utachangia kujenga taasisi imara zinazoweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuaminika mbele ya jamii na wadau wa maendeleo.
Ameeleza kuwa lengo kuu la mwongozo huo ni kuainisha taratibu, majukumu, wajibu na mfumo wa uendeshaji wa NaCoNGO ili kuhakikisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika shughuli zote za Baraza, amesisitiza kuwa taasisi yoyote inayotaka kudumu na kuheshimika lazima ijengwe juu ya misingi ya sheria, maadili na mifumo madhubuti ya utendaji.
Aidha, amesifu muundo wa Baraza unaojumuisha wajumbe 30 wanaowakilisha mikoa yote 26 ya Tanzania Bara pamoja na makundi maalum ya watu wenye ulemavu, watoto, vijana na mashirika ya kimataifa, Kwa mujibu wa Gwajima, muundo huo unaonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha ushirikishwaji, usawa na uwakilishi mpana wa wadau wote ndani ya sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali.
Katika hotuba yake, Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa mgawanyo sahihi wa majukumu kati ya ngazi za Wilaya, Mkoa na Taifa, amesema mwongozo huo umeweka wazi mamlaka ya kila ngazi na namna ya kushirikiana kwa lengo la kuondoa migongano ya kiutendaji, kuongeza ufanisi na kuimarisha uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Baraza.
Pia ameeleza kuwa toleo hilo la pili limeandaliwa kwa kuzingatia mabadiliko ya kisheria, mazingira ya sasa ya utendaji pamoja na mahitaji mapya ya wanachama na wadau, ameongeza kuwa mwongozo huo ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuimarisha uongozi na utendaji wa NaCoNGO katika kipindi hiki cha maendeleo na mageuzi ya taasisi.
Dkt. Gwajima ametoa pongezi kwa viongozi na wanachama wa NaCoNGO kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza maendeleo ya wananchi, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yana mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za kijamii, utetezi wa haki za makundi mbalimbali na kuimarisha ustawi wa jamii, hivyo yanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Akihitimisha hotuba yake, Waziri Dorothy Gwajima alitoa wito kwa wajumbe na wadau wote wa sekta kuutumia mwongozo huo kama chombo cha kuimarisha mshikamano, uwajibikaji na ushirikiano, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na NaCoNGO katika kujenga sekta imara, yenye kuaminika na yenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi kwa ujumla.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...