-Ni inayozungumzia usafirishaji dawa za kulevya katika vyombo vya usafiri


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

FILAMU iliyopewa jina la Kifurushi ambayo inalenga kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu mapambano dhidi ya dawa za kulevya imezinduliwa rasmi na itakuwa inaoneshwa katika mabasi yote yanayosafiri mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza leo Juni 12,2026 katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema mamlaka hiyo ilifanya majadiliano na LATRA na Bodi ya Filamu Tanzania na kuona umuhimu wa kuandaa filamu itakayooneshwa katika mabasi yote yanayosafiri mikoa kmbalimbali nchini.

Amesema hatua hiyo ni kama moja ya njia ya kutoa elimu kwa jamii ili kuzuia athari zinazoweza kusababishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.Filamu hiyo fupi imeandaliwa kuonesha uhalisia wa namna ambavyo mtu anaweza kuingia kwenye mtego wa kuwa sehemu ya wahalifu, kusafirisha dawa za kulevya kwa kubeba.

“Au kusafirisha mzigo auvifurushi asivyovifahamu pamoja na kutambua madhara ya kijamii na kiuchumi yanayoweza kujitokeza kutokana na kitendo hicho.Ni kwa msingi huo tumekuja na ‘’Kaulimbiu isemayo, Usafiri Salama bila dawa za kulevya.

Aidha amesema filamu hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa madereva,makondakta, wahudumu wa mabasi, wasafirishaji wa mizigo, abiria na wananchi kwa ujumla kuhusu wajibu wao katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za vitendo vinavyohusiana na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Akieleza zaidi kuhusu sababu za kuja na filamu hiyo amesema dawa za kulevya ni tishio kubwa kwa afya za wananchi, ustawi wa familia, usalama wa jamii na maendeleo ya taifa letu na kwamba madhara ya dawa za kulevya yanachangia kuongezeka kwa changamoto za kiafya, uhalifu, kuzorota kwa familia, uvunjifu wa amani, pamoja na kudhoofika kwa nguvu kazi ya taifa, hususan vijana na hatimaye huathiri maeneo muhimu ya kiuchumi.

“Kutokana na athari hizo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya.”

Amefafanu hatua hizo zinajumuisha operesheni za ukamataji, tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, uchunguzi wa makosa ya dawa za kulevya pamoja na utoaji wa elimu kwa umma ili kujenga uelewa na ushiriki wa wananchi katika mapambano haya.

Ameongeza pia kwa siku za hivi karibuni, Mamlaka imeendelea kubaini mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo kupitia vyombo vya usafiri wa umma.

“Mara nyingi dawa hizo hufichwa kwenye mizigo na vifurushi vinavyoonekana kuwa vya kawaida.Baadhi ya wananchi, abiria na hata wahudumu wa ndani ya vyombo vya usafiri wamejikuta wakihusishwa na makosa ya dawa za kulevya baada ya kubainika kubeba mizigo wasiyoifahamu.

“Ninitumie fursa hii kuwaomba wamiliki wa mabasi, makampuni ya usafirishaji na wadau wote wa sekta ya usafiri kuipokea na kuipa kipaumbele filamu hii kwa kuhakikisha inaoneshwa katika vyombo vyao vya usafiri.

“Ushirikiano wenu utasaidia kuwafikia kwa haraka wananchi wengi kila siku na kufanya kila safari kuwa fursa ya kutoa elimu na kuimarisha usalama wa jamii dhidi ya tatizo la dawa za

kulevya.Tumechagua kuzindua filamu hii hapa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kwa sababu ni moja ya kituo kikubwa zaidi nchini kinachohudumia maelfu ya wasafiri kila siku.”

Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa ujumbe kwa jamii ya Watanzania kwamba “Usikubali kubeba mzigo, kifurushi au bidhaa yoyote usiyoifahamu. Hakikisha unatambua unachobeba, kinatoka kwa nani na kinaelekea kwa nani. Kifurushi unachodhani ni cha kawaida kinaweza kubeba dawa za kulevya na kubadili maisha yako kwa matokeo hasi”.

Ameongeza kwa pamoja tunaweza kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya, kulinda vijana wetu, kuimarisha usalama wa jamii na kujenga Taifa lenye afya, nguvu kazi salama na maendeleo endelevu kupitia ujumbe uliopo kwenye filamu hiyo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...