Na mwandishi wetu, Zanzibar.
Katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita la kukuza uchumi kwa wananchi wake Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imeamua mpango kabambe ya kuhakikisha inaboresha soko lake la bidhaa pamoja na huduma mbalimbali lililopo katika Mji wa Mbalizi Tarafani ili kuchochea zaidi shughuli za kiuchumi na kuongeza hali ya ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya kuharakisha kwa kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo.
Mpango huo umekuja kufuatia ziara ya baraza la madiwani pamoja na jopo la wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, waliozuru visiwani Zanzibar, kuanzia tarehe 01 hadi 04 Juni 2026, kwa ajili ya mafunzo mbalimbali kuhusu mifumo ya uongozi katika sekta ya uchumi na kijamii kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia fursa zinazowazunguka katika maeneo yao husika ya kiutawala.
Ziara hiyo ya mafunzo ilifanyika katika Baraza la Manispaa ya Magharibi B, inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Sabra Issa Machano, ambapo ugeni wa baraza la madiwani na wataalam wanaounda menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, walipata fursa ya kutembelea masoko makubwa mawili: Soko la Mwanakwerekwe na Soko la Jumbi.
Soko la Mwanakwerekwe ni soko lilijengwa baada ya kushirikisha wadau pamoja na uwezeshaji kupitia mkopo kutoka sekta binafsi kisha baadae serikali kuu kutoa fedha kwa ajili ya kumaridhia mradi huo.
Soko hilo linabeba wafanyabiashara takribani 5,224 tofauti na awali kabla ya kuboreshwa, ambapo lilikuwa linabeba wafanyabiashara 3,000 pekee. Uboreshaji huo umevutia karibu asilimia 50 ya wafanyabiashara wapya.
“Soko hili linafanya kazi saa 24 na linahudumia takribani watu 50,000 kwa siku. Ujenzi wake umezingatia kila aina ya watu kulingana na mahitaji yao. Hapa kuna maduka 187, vibanda 1,344, meza 152, bucha 18, maghala 12, vibanda vya kuegesha kwa biashara maarufu kama vigoli 56,” ameeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Manispaa ya Magharibi B.
Mfumo huo umewavutia zaidi madiwani pamoja na timu ya wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, waliokuwa katika ziara hiyo na kuweka azimio la kutaka kuboresha soko la Mbalizi, ambalo limekuwa kitovu kikubwa cha kibiashara katika Halmashauri. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica E. Yegella amesema Halmashauri inahitaji kuwa na soko la kisasa kama Mwanakwerekwe na Jumbi kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa Halmashauri na wananchi wake.
Ameeleza kwamba Halmashauri inakusanya mapato ya ndani takribani shilingi bilioni nane (8) kwa mwaka, lakini ipo fursa ya kuboresha soko la Mbalizi hata kwa kupitia ubia na wadau wa maendeleo kutoka sekta binafsi ikiwemo taasisi za kifedha kama vile benki kwa ajili ya kuboresha soko hili linalobeba kiwango kikubwa cha wajasiriamali wakiwemo vijana wa kike na kiume sambamba na wanawake.
“Ziara yetu Zanzibar imekuwa na manufaa makubwa. Sote kama menejimenti na baraza letu la madiwani tumejionea kwa macho. Ipo fursa ya kuongeza mapato kupitia soko letu. Kinachotakiwa ni kuboresha miundombinu ya soko letu. Tuko tayari kuingia ubia na mdau yoyote ambaye anaweza kushirikiana nasi katika kuboresha sehemu hii kwa ajili ya kutengeneza mazingira rafiki ya biashara kwa wajasiriamali wetu.” Amesema Mkurugenzi Mtendaji Bi. Erica E. Yegella.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mhe. Aidda C. Haule, amesema Mji wa Mbalizi unakua kwa kasi kutokana na muingiliano mkubwa wa watu kupitia biashara mbalimbali. Amesema ujenzi wa masoko ya kisasa kama ilivyo kwa Zanzibar itasaidia pia kuhakikisha suala la mipango miji linazingatiwa kikamilifu pasina changamoto tofauti na ilivyo sasa, ambapo wafanyabiashara wametapakaa mpaka barabarani hali inayoleta usumbufu kwa watembea kwa miguu na watu wanaoendesha vyombo vya moto.
“Ziara hii imekuwa na tija kwetu kama Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imetuonesha namna ambavyo tunaweza kushirikiana na wadau kuboresha masoko yetu, ambayo ni vituo muhimu kibiashara. Lakini pia tunaweza kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara pamoja na watoto wao kwa kujenga hata miundombinu ya kulelea watoto ndani ya soko letu kama ambavyo tumeona katika masoko ya hapa Zanzibar.” amesema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Halmashauri Wilaya ya Mbeya imemaliza ziara yake ya siku nne ambapo imewea kutembelea maeneo mbali mbali yaliyopo Visiwani Zanzibra ikiwemo eneo la unguja ambapo madiwani, wataalamu pamoja na Mkurugenzi wameweza kujifunza mambo mbali mbali ambayo yataweza kuwa ni moja ya mkombozi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.


.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...