Na Belinda Joseph-Dodoma.

Wananchi wametakiwa kufahamu hali zao za kiafya mapema kwa kupima viashiria muhimu vinavyohusiana na magonjwa yasiyoambukiza ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na magonjwa hayo bila kuonyesha dalili katika hatua za awali.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Huduma za Utawala kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Joachim Asenga, wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.

Asenga alisema JKCI inashiriki maonyesho hayo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo pamoja na kuhamasisha kampeni ya “Jua Namba Zako”, inayolenga kuwasaidia wananchi kufahamu hali zao za kiafya na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema namba hizo zinahusisha shinikizo la damu, mapigo ya moyo, kiwango cha sukari kwenye damu, uwiano wa uzito kwa urefu pamoja na kiwango cha mafuta kwenye damu.

“Watu wengi huamini wana afya njema kwa sababu hawana dalili zozote, lakini magonjwa mengi yasiyoambukiza huanza kimya kimya bila kuonyesha dalili za awali,  ndiyo maana ni muhimu kwa kila mtu kujua namba zake.”

Alionya kuwa magonjwa hayo yasipotambuliwa mapema yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kiharusi, kupooza, mshtuko wa moyo na figo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Asenga aliwataka wananchi wa Dodoma pamoja na watumishi wa umma wanaoshiriki maonyesho hayo kutembelea banda la JKCI kwa ajili ya kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu bila malipo.

“Niwakaribishe wananchi wote kufika katika banda letu, vipimo vyote vinatolewa bure na ni fursa muhimu kwa mtu kujua hali yake ya afya kabla ya matatizo makubwa kutokea”.

Kwa upande wake, Daktari kutoka JKCI, Daud Geofrey Gwirenza, alisema ndani ya siku tatu za ushiriki wao katika maonyesho hayo, watu takribani 170 wamepatiwa vipimo mbalimbali vya afya huku zaidi ya wagonjwa 20 wakipewa rufaa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.

Alisema takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa wananchi kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini matatizo mapema na kupata huduma stahiki.

Dk. Gwirenza alitaja makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo kuwa ni pamoja na watu wenye uzito uliopitiliza, wenye historia ya presha, kisukari au lehemu katika familia zao, wanaovuta sigara, wenye kisukari na wale walio katika hatari ya kupata kisukari au shinikizo la damu.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...