Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) una mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa taasisi za umma na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kafulila alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mhadhara wa umma uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), akieleza kuwa mataifa mengi duniani yameendelea kuwekeza katika mfumo wa PPP kutokana na manufaa yake katika kuimarisha utendaji wa taasisi na kuongeza tija ya kiuchumi.

Alisema sababu kuu tatu zinazochochea matumizi ya mfumo huo duniani ni kuvutia mitaji ya sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umma, kuongeza ufanisi wa taasisi za serikali na kukuza ubunifu.

“PPP siyo tu njia ya kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, bali ni nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi wa taasisi za umma na kuhamasisha ubunifu unaochangia maendeleo endelevu ya uchumi,” alisema Kafulila.

Alibainisha kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa katika baadhi ya nchi zilizoendelea, takribani asilimia 25 ya utajiri wa taifa unatokana na ufanisi wa taasisi zake, huku rasilimali za asili zikichangia karibu asilimia tano pekee.

Kwa mujibu wa Kafulila, mafanikio ya nchi hizo hayatokani na ukosefu wa rasilimali za asili, bali uwezo wa kujenga mifumo madhubuti inayowezesha matumizi bora ya rasilimali zilizopo.

Alitolea mfano nchi za China, Marekani na Urusi ambazo pamoja na kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za asili, zimejikita zaidi katika kuimarisha rasilimali watu, ubunifu na taasisi zenye ufanisi mkubwa.

“China inazalisha dhahabu nyingi kuliko nchi yoyote Afrika, Marekani ina mafuta mengi kuliko mataifa mengi duniani na Urusi ina gesi nyingi kuliko nchi yoyote Afrika. Hata hivyo, msingi wa maendeleo yao ni nguvu ya taasisi, ubunifu na rasilimali watu,” alisema.

Kafulila alisisitiza kuwa Tanzania inaweza kunufaika zaidi na mfumo wa PPP kwa kutumia sekta binafsi kama mshirika wa maendeleo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, huku ikiimarisha ufanisi wa taasisi za umma na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...