Na. Calvin Katera - Arusha.

Maonesho ya Karibu- KiliFair yameendelea kuwa na umuhimu mkubwa kwa TANAPA kwani ni jukwaa la kuwakutanisha wadau wa ndani na nje ili kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa nchini. Kupitia maonesho hayo, TANAPA hukutana na wadau mbalimbali wa utalii wa ndani na nje ambao wameendelea kuwekeza na kuchagiza ongezeko la watalii katika Hifadhi za Taifa nchini.

Akifungua Maonesho hayo leo juni 05, 2026 katika Viwanja vya Magereza jijini Arusha, Mkurugenzi wa Utalii Dkt. Thereza Mugobi kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa Karibu-KiliFair ni zaidi ya maonesho, vilevile ni uwekezaji wa kimkakati katika mustakabali wa utalii wa Tanzania. 

Uhusiano huu wa kibiashara ulioanzishwa katika jukwaa hili la Karibu KiliFair umezalisha ushirikiano mpya, kuongeza idadi ya watalii wanaowasili nchini, kuvutia uwekezaji, kutengeneza ajira, na kuimarisha maisha ya jamii zinazotegemea utalii. 

"Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya utalii ikiwemo malazi, viwanja vya ndege, barabara ili kuboresha uzoefu wa watalii na kuwafikisha katika maeneo mbalimbali yenye vivutio kwa urahisi. Aidha, Wizara itaendelea kutangaza vivutio vyake kupitia njia za kidijitali ili kuyafikia masoko mbalimbali duniani." Alisema Dkt. Mugobi.

Naye, mwakilishi kutoka “TATO” Wilbard Chambulo, alisema kuwa maonesho haya ni daraja linalounganisha wadau wa ndani ambao ni mawakala wa utalii na waongoza watalii pamoja na mawakala wa kimataifa kutoka katika mabara yote duniani.

Sanjari na hayo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Dkt. Beatrice Kessy kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA aisema; “Karibu-KiliFair huimarisha ushirikiano kati ya TANAPA na wadau wa sekta ya utalii duniani. 

Kupitia mikutano na majadiliano ya kibiashara, TANAPA hujenga mahusiano mapya, hujifunza mwenendo na muelekeo wa masoko ya utalii na uwekezaji ili kupanua wigo wa uwekezaji na kukuza utalii nchini.”

Ushiriki wa TANAPA katika Karibu-KiliFair unaendelea kuwa chachu ya kutangaza vivutio vya utalii, kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya utalii, pamoja na kuvutia watalii na wawekezaji zaidi kutembelea na kuwekeza katika Hifadhi za Taifa Tanzania.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...