Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Serikali imewataka Maafisa Utumishi na Wasimamizi wa Rasilimaliwatu nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma ili kuimarisha utoaji wa huduma na kupunguza malalamiko kutoka kwa watumishi pamoja na wananchi.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, wakati akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
Qwaray amesema Serikali inatarajia watumishi wa umma kusimamia haki za watumishi kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha masuala yanayohusu maendeleo ya kiutumishi yanashughulikiwa kwa wakati. Amesisitiza kuwa malalamiko ya kutopandishwa madaraka, ucheleweshaji wa haki za watumishi na ukiukwaji wa maadili ya kazi yanapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuimarisha mazingira bora ya utendaji kazi katika taasisi za umma.
Aidha, amewataka viongozi wa rasilimaliwatu kuhakikisha watumishi wanapatiwa mafunzo kuhusu usalama wa taarifa za Serikali na matumizi sahihi ya Akili Unde (AI) kwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma. Pia amesisitiza matumizi ya barua pepe rasmi za Serikali katika mawasiliano yote ya kikazi na kuonya kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya watumishi watakaotumia vibaya mifumo hiyo au teknolojia ya Akili Unde kinyume cha taratibu zilizowekwa.
Katika hatua nyingine, Qwaray ameonyesha wasiwasi wake kuhusu dosari zinazojitokeza katika uendeshaji wa mashauri ya nidhamu, akisema baadhi ya waajiri wamekuwa hawafuati taratibu za kisheria hali inayosababisha watumishi waliotiwa hatiani kushinda rufaa zao. Amesema hali hiyo inaigharimu Serikali fedha nyingi na kuathiri taswira ya Utumishi wa Umma, hivyo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu katika kushughulikia mashauri hayo.
Kuhusu utekelezaji wa Mfumo wa e-Utendaji, Naibu Waziri huyo amesema viongozi wa rasilimaliwatu wanapaswa kuhakikisha watumishi wanapatiwa mafunzo ya kutosha ili kuutumia mfumo huo kwa ufanisi. Amesikitishwa na taarifa za baadhi ya wasimamizi kushindwa kufanya tathmini za utendaji kazi kwa mwaka 2024/2025, jambo lililosababisha baadhi ya watumishi kunyimwa haki zao za maendeleo ya kiutumishi.
Kutokana na hali hiyo, amemuelekeza Katibu Mkuu (Utumishi) kwa kushirikiana na waajiri kuwabaini wasimamizi walioshindwa kutekeleza wajibu wao na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Pia amesisitiza kuwa watumishi walioathirika kutokana na uzembe wa wasimamizi wao wasikwamishwe katika maendeleo yao ya kiutumishi.
Hata hivyo Qwaray amewataka watumishi wote Nchini kukamilisha kwa wakati majukumu yao katika Mfumo wa e-Utendaji kabla ya Juni 30, 2026, huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi na wasimamizi watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...