Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

TANZANIA na Malaysia zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika elimu ya juu kupitia ubia wa vyuo vikuu, tafiti za pamoja, ubadilishanaji wa wanafunzi na wahadhiri, ufadhili wa masomo pamoja na ushirikiano katika sayansi na teknolojia.

Vyuo Vikuu tisa vimeanza maonesho ya elimu katika Hoteli ya Serena kwa kutoa elimu na fursa ya watanzania kupata elimu katika nchi hiyo.

Akizungumza katika kikao cha Kuimarisha Ushirikiano wa Elimu ya Juu Kati ya Tanzania na Malaysia kilichofanyika Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi amesema ujio wa ujumbe wa elimu kutoka Malaysia ni wa wakati muafaka wakati Tanzania ikiendelea kuimarisha na kutangaza kimataifa mfumo wake wa elimu ya juu.

Kikao hicho kiliandaliwa na kuratibiwa na Education Malaysia Global Services (EMGS) chini ya Wizara ya Elimu ya Juu ya Malaysia kwa kushirikiana na Global Education Link (GEL). Prof. Mushi amesema ujio wa ujumbe huo umevitambulisha vyuo vya Malaysia nchini Tanzania na kutoa nafasi kwa pande zote mbili kujadili maeneo ya ushirikiano yatakayowanufaisha wanafunzi, wahadhiri na taasisi za elimu ya juu.

Amesema Tanzania inatarajia kuona ushirikiano utakaoimarisha programu za pamoja, kubadilishana maarifa, tafiti, ubunifu na kuongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu nchini.

Aidha, amesema Malaysia imepiga hatua kubwa katika kutumia elimu, teknolojia na ujuzi kama nyenzo ya mageuzi ya kiuchumi, jambo ambalo Tanzania inaweza kujifunza katika safari yake ya kujenga uchumi unaotegemea maarifa na teknolojia.

Kwa mujibu wa Prof. Mushi, kipaumbele kinapaswa kuwekwa katika kuwaandaa wanafunzi wa Tanzania kwenye maeneo ya sayansi, hisabati, kemia, sayansi ya takwimu, ujifunzaji wa mashine na akili mnemba.

Amesema wanafunzi wanaotaka kusoma nje ya nchi wanapaswa kuandaliwa si kitaaluma pekee bali pia kilugha na kitamaduni ili waweze kushindana katika mazingira ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Stephen Maluka amesema kikao hicho kimetoa jukwaa la vitendo kwa taasisi za Tanzania na Malaysia kujadili namna bora ya kujenga ushirikiano rasmi katika elimu, sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel amesema GEL inajivunia kuratibu mpango huo unaounganisha taasisi za Tanzania na vyuo vikuu pamoja na mamlaka za elimu kutoka Malaysia. Amesema ushirikiano huo unalenga kujenga daraja la kweli kati ya Tanzania na Malaysia katika elimu ya juu kupitia tafiti, programu za kitaaluma, ubadilishanaji wa wanafunzi na wahadhiri pamoja na mafunzo yanayotegemea teknolojia.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...