Mwanza.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kupitia mradi wa RISE imehitimisha mafunzo ya Wakufunzi Wasaidizi (Training of Trainers – ToTs) yaliyowashirikisha wataalamu wa TARURA pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa matengenezo ya kawaida ya barabara kupitia vikundi vya kijamii.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhandisi Richard Missa kutoka TARURA alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo maafisa na wadau watakaosimamia utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika matengenezo ya barabara huku wakinufaika kiuchumi kupitia ajira na shughuli za matengenezo ya mara kwa mara.
"Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya utunzaji wa miundombinu ya barabara huku wakiongeza kipato chao. Zoezi hili ni endelevu na linahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa", amesema Mhandisi Missa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya mradi wa RISE kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhandisi Emmanuel Mhiliwa, amesema serikali ina imani kuwa wataalamu wote waliopata mafunzo hayo watakwenda kuyatumia kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuhakikisha vikundi vya kijamii vinafanya kazi kwa weledi.
"Kuna mawazo ya wananchi kuwa barabara ni mali ya TARURA au TANROADS pekee, wakati ukweli ni kwamba barabara ni mali ya wananchi wote, ndiyo maana tunaunda vikundi hivi vya kijamii ili wananchi washiriki moja kwa moja katika kutunza barabara. Hii itawajengea hisia ya umiliki wa miradi, kuongeza ajira, kulinda miundombinu hiyo na kuhakikisha inadumu kwa manufaa yao", amesema.


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...