Na Diana Byera.

Vijana wa timu 20 wanaotokea Tarafa ya Kamachumu, wilayani Muleba mkoani Kagera, wanatarajia kushindania jumla ya shilingi milioni 6 kupitia mashindano ya Kamachumu Paul Mwijage Cup ambayo yatatimua vumbi kuanzia Juni 10 hadi Julai 15 mwaka huu.

Mkurugenzi wa mashindano hayo, Paul Mwijage, alisema kuwa katika kuhakikisha anaunga mkono serikali katika masuala ya kuibua vipaji vya vijana kupitia michezo, ameamua kuanzisha mashindano hayo ambayo yanalenga kuibua vipaji, kuimarisha mshikamano na kukutanisha vijana pamoja kwa ajili ya agenda zao za michezo.

Alisema kuwa mshindi wa kwanza atajinyakulia shilingi milioni 3, mshindi wa pili milioni 2 na mshindi wa tatu shilingi milioni 1, Pia vifaa vya michezo kama mipira na jezi vitatolewa kwa kila timu, ambapo ameahidi kuwa ligi hiyo itaendelea kuibua vipaji kwa miaka 10 mfululizo.

Ametoa wito kwa wawekezaji kuwekeza katika viwanja kwani tarafa hiyo inakabiliwa na changamoto ya uwanja. Hivyo, anaamini mashindano hayo yatawavutia wawekezaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanaozaliwa katika wilaya ya Muleba na nje ya wilaya hiyo.

“Mashindano haya ni kivutio kikubwa cha uwekezaji, Wakati mashindano yanaendelea, tunapaswa kuwa na sehemu za migahawa mizuri, tunapaswa kuwa na sehemu za kulala nzuri, chakula, na kutangaza utamaduni wetu na asili zetu kupitia mashindano haya, Ni muda sasa wa wadau wa michezo, wazaliwa wa Wilaya ya Muleba na wakazi wa Mkoa wa Kagera, kuunganisha nguvu na kudumisha michezo katika ukanda huu na kufanya uwekezaji pia”.

Katika uzinduzi wa ligi hiyo, mgeni rasmi alikuwa msemaji wa Timu ya Simba Sports Club, Ahmed Ally, ambaye amesema kuna umuhimu mkubwa mno wa kuanzisha mashindano mengi ngazi ya kata, tarafa na wilaya ili kuibua vipaji vya kweli kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Alisema moja ya mambo yanayoweza kuleta radha mpya katika ligi za ndani nchini na nje ya nchi ni kuhakikisha vijana wanajitokeza kwa wingi wakati mashindano haya yanapotangazwa ili kuonyesha vipaji vyao, na kwa namna hiyo watajikuta wanajulikana katika timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu.

Alitoa wito kwa washiriki kuhakikisha wanaonyesha vipaji na kucheza kwa moyo ili waweze kupata muunganisho wa kuendeleza vipaji vyao na kujipatia kipato.

Mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo imezishirikisha timu za Kamachumu Stars na Bulembo katika viwanja vya Kamachumu, ambapo timu ya Bulembo imeshinda kwa mikwaju ya penalti na kujinyakulia medali na shilingi 500,000 kama sehemu ya ufunguzi wa michuano hiyo.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...